KENYA

Shirikisho la Soka nchini Kenya lampongeza mchezaji wa Harambee Stars Victor Wanyama kusajiliwa na Southampton

Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars Victor Wanyama
Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars Victor Wanyama

Shrikisho la soka nchini Kenya FKF limempongeza kiungo wa kati wa timu ya taifa ya soka Harambee Stars kwa kusajiliwa na klabu ya Uingereza ya Southampton.

Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa FKF Sam Nyemweya amesema Wanyama ambaye msimu uliopita alikuwa anachezea Celtic ya Scotland ameweka historia kuwa mchezaji wa kwanza kutoka nchini humo na Kanda ya Afrika Mashariki kusajiliwa na klabu ya Uingereza.

Uongozi wa soka nchini Kenya umekuwa ukimsifu Wanyama kwa kujitolea na kuhudhiria mechi zote za timu ya taifa na kuonesha mfano mzuri kwa wachezaji chipukizi nchini humo.

Hata hivyo, uongozi wa Celtic na Southampton haujathibitisha kusajiliwa kwa Wanyama mwenye umri wa miaka 22.

Kumekuwa na taarifa kuwa mchezaji huyo wa Kimataifa wa Kenya anatarajiwa kujiunga na Southampton kwa kitita cha Pauni Milioni 12 .

Wiki iliyopita kocha wa Southampton Mauricio Pochettino alithibitisha kuwa alikuwa mbioni kumsajili Wanyama ambaye amekuwa katika klabu ya Celtic kwa kipindi cha miaka miwili sasa.

Mwaka 2010 kaka yake Wanyama, Macdonald Mariga alishindwa kujiunga na Manchester City baada ya kukosa cheti cha kufanya kazi nchini humo kwa sababu Kenya ilikuwa chini ya orodha ya timu 70 duniani katika orodha ya FIFA kwa mujibu wa sheria za soka nchini humo ili kufanikisha usajili.