MICHEZO

Stars na The Cranes kumenyana leo uwanja wa Taifa Dar es Salaam

Kikosi cha timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars
Kikosi cha timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars www.24tanzania.com

Timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars leo Julai 13 inashuka dimbani majira ya saa tisa alasiri kumenyana na timu ya taifa ya Uganda (The Cranes)katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini. 

Matangazo ya kibiashara

Mtanange huo utapigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo mamia ya mashabiki na wadau wa soka wanatarajiwa kujitokeza kushuhudia mpambano huo.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameibariki Stars na kusema kuwa kikosi hicho kwa sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.

Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga amewaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
Aidha walimu wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya leo itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.