SOKA

Taifa Stars yaambulia kipigo cha bao 1-0 toka kwa The Cranes

Timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars imeambulia kipigo cha bao moja bila toka kwa Uganda The Cranes katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za CHAN iliyopigwa siku ya jumamosi jijini Dar es salaam.

Matangazo ya kibiashara

Bao pekee la ushindi kwa Uganda lilipachikwa katika dakika ya 46 na Dennis Iguma aliyemalizia vizuri krosi aliyoipokea toka kwa mchezaji machachari Brian Majwega.

Akizungumza baada ya kutamatika kwa mechi hiyo Kocha wa The Cranes Milutin Sredojevich ‘Micho’ amewapongeza wachezaji wake na ameahidi kufanya vizuri zaidi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa nchini Uganda baada ya majuma mawili.

Uganda inatakiwa ipate hata sare katika mchezo wa marudiano dhidi ya Stars ili waweze kufuzu kuelekea nchini Afrika Kusini kwenye fainali za CHAN hapo mwakani.

Kwa upande wake kocha wa Stars Kim Poulsen amewalaumu wachezaji wake kutofunga mabao kutokana na kutotumia vizuri nafasi kadhaa walizopata uwanjani hapo, huku akiwalinganisha na wenzao wa Uganda ambao hawakupata nafasi nyingi kama zao.