RIADHA

Adidas yasitisha mkataba na mwanariadha Tyson Gay, polisi wa Italia wavamia chumba cha mwanariadha, Asafa Powell

Tyson Gay (Kushoto), Nickel Ashmeade (katikati) na Asafa Powell (kulia) kwenye moja ya mashindano yaliyofanyika mwaka huu
Tyson Gay (Kushoto), Nickel Ashmeade (katikati) na Asafa Powell (kulia) kwenye moja ya mashindano yaliyofanyika mwaka huu REUTERS/Ruben Sprich

Siku moja baada ya shirika la Marekani linalopambana na kupiga vita matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mchezoni kutangaza kuwa mwanariadha Tyson Gay alitumia dawa za kusisimua misuli kwenye moja ya mashindano, kampuni ya Adidas imetangaza kucahana nae.  

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa kampuni ya Adidas amewaambia wanahabari kuwa wameshtushwa na taarifa kuwa mwezi May mwaka huu mwanariadha huyo alitumia dawa za kusisimua misuli wakati aliporejea baada ya kuwa majeruhi.

Msemaji huyo amesema kuwa kwasasa wanasitisha mkataba wa udhamini na mwanariadha huyo na kwamba mpaka pale itakapoamualiwa vinginevyo ndipo watakapofikiria upya kurejesha mkataba wao.

Hapo jana mara baada ya kutangazwa kwa uchunguzi huo ambao pia ulimtaja mwanariadha wa Jamaica Asafa Powell, polisi nchini Italia walivamia hoteli alimokuwemo mwanariadha huyo.

Polisi wa Italia walichukua baadhi ya dawa alizokuwanazo Powell kwaajili ya kuchukua vipimo vya maabara kubaini iwapo zinazuiliwa kutumiwa na wanamichezo.

Taarifa hiyo imekuwa pigo kwa wanariadha hao ambao walianza kurejea kwenye kiwango ambapo wote kwa pamoja wamekanusha kutumia dawa hizo kwa makusudi na kwamba pengine walizitumia bila kufahamu.

Baadhi ya wanariadha wakongwe wamewakosoa wanariadha hao na kudai kuwa hata kama walikuwa hawafahamu hawakupaswa kutumia dawa hizo kwakuwa zinatumika kusisimua misuli.

Kwa upande wake Tyson Gay amesema anatamani sana kukimbia tena lakini kwasasa anasubiri adhabu ambayo atapewa na kwamba yuko tayari kwa lolote.