MPIRA WA MIGUU - UINGEREZA

Wyne Rooney achukizwa kuwa chaguo la pili la kocha mpya, David Moyes

Mshambuliaji Wyne Rooney akifunga moja ya mabao bora zaidi kwenye ligi kuu ya Uingereza
Mshambuliaji Wyne Rooney akifunga moja ya mabao bora zaidi kwenye ligi kuu ya Uingereza

Mshambuliaji wa Manachester United, Wyne Rooney inaelezwa amechukizwa na kauli ya kocha wake David Moyes kudai kuwa atamtumia kama mchezaji wa akiba katika msimu ujao wa ligi.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa toka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa Rooney ameshazungumza na viongozi wa juu wa klabu hiyo kuhusu mustakabali wake katika kikosi cha kwanza na kuweka wazi kuwa hayuko tayari kucheza nyuma ya mshambuliaji Robin Van Persie.

Toka kuwasili kwa Van Persie msimu uliopita akitokea Arsenal, aliyekuwa kocha wa timu hiyo Sir Alex Ferguson alikuwa akimuacha Rooney Benchi na kumuingiza kipindi cha pili hali ambayo dhahiri ilionekana kumkera mchezaji huyo.

Mwisho wa juma hili kwenye mahojiano maalumu, kocha wa Man utd, David Moyes alisisitiza kutomuuza Wyne Rooney na kwamba bado anahitajika sana kwenye klabu hiyo.

Kilichomkera Rooney kinaonekana ni matamshi ya Moyes kuwa atakuwa akimuhitaji mshambuliaji huyo pindi Van Persie akiumia.

Kabla ya kumalizika kwa msimu uliopita, Rooney aliandika barua kuomba klabu yake imuuze lakini ikashindikana kutokana na viongozi wake kumtaka aendelee kubakia kwenye timu yao.

Mshambuliaji huyo anahusishwa na kutaka kujiunga na mahasimu wa Man utd klabu ya Chelsea ama Arsenal ingawa wachambuzi wa masuala ya soka wanasema kuwa iwapo mchezaji huyo atauzwa hatouzwa nchini Uingereza.