MPIRA WA MIGUU - UINGEREZA

Moyes: Rooney ataendelea kusalia kuwa mchezaji wa Man Utd

Kocha mkuu wa klabu ya Manchester United ya nchini Uingereza, David Moyes ameendelea kusisitiza kuwa mshambuliaji wake Wyne Rooney hauzwi na ataendelea kusalia mchezaji wa timu hiyo.

Wyne Rooney akiwa na wenzake wakati alipofanya ziara nchini Thailand
Wyne Rooney akiwa na wenzake wakati alipofanya ziara nchini Thailand Reuters
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari mjini Sydney ambako timu hiyo imeweka kambi yake kwa  sasa, Moyes amesema msimamo wa klabu hiyo haujabadilika kuhusu mshambuliaji wao na kwamba hauzwi.

Kauli ya Moyes inakuja ikiwa zimepita siku chache toka klabu ya Chelsea pia ya Uingereza kutangaza hadharani nia yake ya kumsajili mshambuliaji huyo.

Hata hivyo maombi ya Chelsea yalikataliwa ma uongozi wa Man utd ambao umeendelea kusisitiza kuwa Wyne Rooney hauzwi msimu huu hata kama mkataba wake wake umesalia miaka miwili.

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho aliweka wazi nia yake ya kutaka kumsajili Rooney na kwamba lengo lake kubwa ni kumnasa mshambuliaji huyo huku akisema ikiwa atakua chaguo la pili kwenye klabu yake huenda akapoteza nafasi kwenye timu ya taifa.

Mpaka sasa Rooney mwenyewe ameshaandika barau zaidi ya mara mbili kuuomba uongozi wake umuuze na kwamba hawezi kuwa chaguo la pili nyuma ya Robin Van Persie.

Man utd hivi sasa imeelekeza nguvu zake katika kumnasa kiungo wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Cesc Fabregas.

Dau la Man utd kumtaka Fabregas limeshakataliwa na Barcelona ingawa Moyes anaimani ya kumnasa huku harakati za kumpata Marouane Fellaini na Leighton Baines zikiendelea.