SOKA

Klabu ya Manchester United yatoa ofa ya kitita cha £30 milioni kwa ajili ya kumsajili Kiungo wa Barcelona Cesc Fabregas

Kiungo wa Barcelona Cesc Fabregas akishangilia goli akiwa pamoja na Mshambuliaji Lionel Messi
Kiungo wa Barcelona Cesc Fabregas akishangilia goli akiwa pamoja na Mshambuliaji Lionel Messi Reuters

Klabu ya Manchester United kwa mara nyingine imepeleka ofa yenye thamani ya pauni milioni thelathini kwa timu ya Barcelona wakitaka sini ya Kiungo wa Kimataifa wa Uhispania anayekipiga Camp Nou Cesc Fabregas. Manchester United imeamua kupeleka ofa nyingine kwa Barcelona baada ya hapo awali kutangaza kutoa kitita cha pauni milioni ishirini na tano kwa ajili ya kumsajili Fabregas lakini wakakataliwa.

Matangazo ya kibiashara

Kocha Mkuu wa Manchester United David Moyes amesema Makamu Mwenyekiti Ed Woodward ndiye anayehusika kuhakikisha kuhakikisha Fabregas anasajili ili kuongeza kuimarisha kikosi chao.

Moyes ametoa kauli hiyo alipokutana na waandishi wa habari huko Yokohama ambapo Manchester United ipo kwenye mazoezi yao ya mwanzoni mwa msimu nchini Japan huku mikakati ya kuimarisha timu hiyo ili kutetea Ubingwa wake ikiendelea.

Kocha Mkuu wa Manchester United amesema iwapo unamhitaji mchezaji mzuri kuna wakati lazima mtumie juhudi za ziada katika kuhakikisha mnapata saini yake kwa kuwa timu nyingine nazo zinakuwa zinamhitaji.

Moyes amekiri Manchester United inamhitaji kwa nguvu zote Fabregas ambaye wanaimani ataweza kuwasaidia kuimarisha sehemu ya kiungo ambayo inahitaji mbadala wa Paul Scholes aliyetundika daruga.

Juma lililopita aliyekuwa Kocha Mkuu wa Barcelona Tito Vilanova aliweka bayana Fabregas anataka kuendelea kusalia Camp Nou na hana mpango wa kuondoka na kujiunga na timu yoyote nyingine.

Fabregas alianzia soka yake katika Chuo Cha Soka cha La Masia kabla ya kujizolea umaarufu na baadaye kusajiliwa na Arsenal ambako alifikia hatua ya kuwa nahodha kabla ya kurejea tena Barcelona.

Kiungo huyo wa Kimataifa wa Uhispania Fabregas aliitumikia Arsenal kwa kipindi cha miaka nane na kucheza michezo 303 huku akiweza kufunga magoli 57 kabla ya kusajili mkataba wa miaka mitano na Barcelona mwaka 2011.