SOKA

Kocha Mkuu wa Liverpool Brendan Rodgers akiri bado anamhitaji Luis Suarez aliyeonsha nia ya kuondoka Anfield

Mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez ambaye ameweka bayana nia yake ya kuondoka Anfield
Mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez ambaye ameweka bayana nia yake ya kuondoka Anfield REUTERS/Phil Noble

Kocha Mkuu wa Liverpool Brendan Rodgers amekiri hamu yake kubwa ni kuendelea kumuona Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uruguay Luis Suarez anaendelea kusalia Anfield kwa ajili ya msimu ujao licha ya kwamba mwenyewe ameshikilia msimamo wa kutaka kuuzwa. Suarez ambaye alishika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora msimu uliopita nyuma ya Robin Van Persie wa Manchester United ameweka bayana dhamira yake ya kuhama nchini Uingereza akisema amekuwa akiandamwa mno na waamuzi lakini pia anataka kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Mshambuliaji huyo amesema angependa kucheza katika Ligi Kuu nchini Uhispania maarufu kama La Liga na amekiri amechoshwa na tabia za vyombo vya habari nchini Uingereza kumuandama na kuchangia maisha yake kuwa magumu mno.

Suarez ambaye msimu uliopita alifunga magoli 23 ameshajiunga na wachezaji wenzake kwenye kikosi cha timuhiyo kilichopo nchini Australia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao licha ya kwamba anataka kukihama kikosi cha Liverpool.

Rodgers amewaambia wanahabari huko Melbourne kwamba anamhitaji sana Suarez kuendelea kuwepo Liverpool msimu ujao kwani amekuwa mchango mkubwa kwenye mafaniko ya timu hiyo msimu uliopita.

Kocha huyo wa Vijogoo Vya Jiji amesema licha ya kuwepo wa taarifa za Suarez kutaka kuondoka lakini bado amekuwa na thamani kubwa kwa Liverpool kitu ambacho kinamsukuma kukiri bado amekuwa nguzo ya safu ya ushambuliaji.

Rodgers amesema Suarez amejiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya maandalizi ya mwanzoni mwa msimu baadaya kupata mapumziko ya kutosha na wanaimani atakuwa tayari kuitumikia timu hiyo.

Suarez alijiunga na Liverpool akitokea Ajax Amsterdam mwezi january mwaka 2011 na kuwa na kipindi kizuri licha ya kwamba aliingia kwenye mtafaruku baada ya kumbagua Patrice Evra na kisha kumng'ata Branislav Ivanovic.

Mshambuliaji huyo baada ya kumaliza msimu wa Ligi Kuu nchini Uingereza aliweka bayana anataka kuondoka Liverpool na iwapo Real Madrid watakuwa wanamhitaji hatosita kujiunga nao.