SOKA-CAF

Recreativo de Libolo yaanza kwa ushindi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuifunga Esperance katika Kundi B

Nembo inayotumika kutambulisha Mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika CAF
Nembo inayotumika kutambulisha Mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika CAF

Mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Afrika CAF yameanza na kushuhudia matokeo ya kushtua baada ya Timu ya Recreativo Libolo ya Angola kuanza hatua hiyo kwa kuwafunga Esperance ya Tunisia kwa goli 1-0. Goli la pekee la Recreativo lilifungwa katika dakika tatu za majeruhi na hivyo kuwafanya waongoeze Kundi B kutokana na mchezo mwingine wa Kundi hilo kati ya Coton Sport ya Cameroon na Sewe Sport ya Cote D'Ivoire kutochezwa.

Matangazo ya kibiashara

Mshambuliaji wa Recreativo aliyeingia kipindi cha pili Aguinaldo ndiye alikwamisha mpira huo nyavuni baada ya hapo awali kukosa nafasi nyingi za wazi kutokana na wachezaji wenzake kutokuwa makini.

Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Manispaa uliopo katika Mji wa Calulo ambao unapatikana umbali wa kilometa 220 kutoka Mji Mkuu Luanda na hivyo Recreativo kuonekana kuanza vizuri hatua ya makundi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Recreativo kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kwenye mchezo huo mlinda mlango wake Landu alionekana nyota ya mchezo.

Esperance licha ya kuwatumia wachezaji wake wenye uzoefu wakiwemo Moez Ben Cherifia na Khaled Mouelhi lakini hawakuambua kitu na hivyo mchezo huo ukamalizika kwa wao kupata kichapo cha ugenini.

Recreativo ilifanikiwa kutinga hatua hiyo ya Ligi Ndogo baada ya kuwaondosha Simba ya Tanzania kabla ya kuwashinda El-Merreikh ya Sudan na mwisho waliondosha Enugu Rangers ya Nigeria.

Katika mchezo mwingine wa Kundi A ulishuhudia Orlando Pirates wakiwa nyumbani wakilazimishwa sare ya kutofungana na AC Leopards ya Congo katika mchezo uliokuwa na upinzani mkubwa.

Ratiba ya michezo mingine ya hatua ya Ligi Ndogo inatarajia kushuhudia Zamalek akikabiliana na Mabingwa Watetezi Al Ahly siku jumatano mchezo uliosogezwa mbele kutokana na mchafuko yanyoendela nchini Misri.

Mchezo mwingine wa Kundi B kati ya Coton Sport ya Cameroon dhidi ya Sewe San Pedro ya Cote D'Ivoire unatarajiwa kupigwa siku ya jumamosi baada ya hapo mwanzo kuzuiliwa baada ya Cameroon kufunguliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA.