SOKA-FIFA-CAMEROON

FIFA yaiondolea adhabu Chama Cha Soka nchini Cameroon Fecafoot baada ya kuundwa kwa Kamati Maalum kushughulikia mgogoro

Nembo cha Shirikisho la Soka Nchini Cameroon Fecafoot
Nembo cha Shirikisho la Soka Nchini Cameroon Fecafoot

Shirikisho la Soka Duniani FIFA limeondoa adhabu ya kuifungia Cameroon kushiriki mashindano yoyote kutokana na kuundwa kwa Kamati Maalum ambayo itaongoza kwa muda ili kushughulikia mgogoro uliozuka ndani ya Chama Cha Soka Fecafoot.

Matangazo ya kibiashara

FIFA imefikia uamuzi wa kuondoa adhabu iliyokuwa imeiweka kwa Cameroon kutokana na kuundwa kwa Kamati hiyo itakayokuwa inaongozwa na Waziri wa zamani Elimu na Michezo Joseph Owona kusaka suluhu ya mgogoro uliozuka.

Cameroon ilifungiwa mapema mwezi huu kutokana na Serikali kuingilia shughuli za uendeshaji wa soka kitu ambacho kimekuwa kikipingwa vikali na FIFA na hivyo wakachukua uamuzi wa kuifungia kushiriki kwenye mchezo wa soka.

Kamati hiyo itakuwa chini ya uangalizi wa FIFA kupitia Mjumbe wake Primo Carvaro pamoja na Mwakilishi wa Chama Cha Soka Barani Afrika CAF Prosper Abega wakiwa na kibarua cha kuhakikisha uchaguzi Mkuu unaitishwa upya.

Uamuzi wa FIFA kuifungulia Cameroon ulikuja baada ya Ujumbe wa nchi hiyo ukiingozwa na Waziri wa Michezo Adoum Garoua kukutana na Rais wa FIFA Sepp Blatter kuangalia ni kwa namna gani mgogoro huo ungeshughulikiwa.

Kamati hiyo Maalum inapaswa pia kuitisha uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini Cameroon Fecafoot ambao unatakiwa kufanyika tarehe 31 ya mwezi Machi mwakani kupata uongozi mpya utakaoongoza soka nchini humo.

Cameroon iliingia matatani baada ya Serikali kumfungulia mashtaka Iya Mohamed ambaye alifanikiwa kushinda kwenye Uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini Cameroon Fecafoot kitu ambacho kililikasirisha FIFA.

Kamati hiyo Maalum inaongozwa na Joseph Owona ambapo Msaidizi wake ni Emmanuel Ngassa Happi pamoja na wajumbe kumi ambao ni Michel Kaham, Ebenezer Mouloke, Ephraim Gwafor, Owona Pascal Bialong,David N'Hanack Tonye, James Moungue Kobila, Jonathan Fombe, Amadou Evele na Adolphe Minkoa.