SOKA

Guus Hiddink atangaza kujiuzulu wadhifa wake wa kuinoa Klabu ya Anzhi Makhachkala ya nchini Urusi

Guud Hiddink amejiuzulu wadhifa wake wa kuinoa Klabu ya Anzhi Makhchkala ya nchini Urusi
Guud Hiddink amejiuzulu wadhifa wake wa kuinoa Klabu ya Anzhi Makhchkala ya nchini Urusi

Guus Hiddink ametangaza kujiuzulu wadhifa wake wa kuinoa Klabu ya nchini Urusi ya Anzhi Makhachkala ambapo nafasi yake imechukuliwa na Kocha wa zamani wa Manchester United Rene Meulensteen.

Matangazo ya kibiashara

Hiddink mwenye umri wa miaka 66 amesema uamuzi wake umekuja kutokana na dhamira aliyokuwa ameiweka hapo awali ya kwamba angeachia wadhifa wake pale ambapo Klabu ya Anzhi ingekuwa na uwezo wa kusimama yenyewe.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea ameweka wazi kabisa malengo yake yameshatimia na ndiyo maana ameamua kujiweka kando na kuiacha Timu hiyo akitaka iendelee kupata mafanikio ambayo yeye ameyaasisi.

Hiddink alipata mafanikio makubwa sana alipokuwa anaifundisha Klabu ya PSV na kuweza kutwaa mataji sita ya Ligi sanjari na mataji mengine manne ya Chama Cha Soka kabla ya kutwaa Taji la Kombe la Ulaya.

Kocha huyo pia aliweza kuinoa Chelsea na kufanikiwa kuipa ubingwa wa Kombe la Chama Cha Soka nchini Uingereza FA mwaka 2009 kabla ya kuondoka na kuelekea nchini Urusi kuchukua kibarua cha kuinoa Anzhi.

Hiddink licha ya kunoa Klabu pekee lakini pia amepata nafasi ya kuzinoa Timu za taifa ikiwemo Uholanzi, Korea Kusini, Australia na Urusi ambako kote aliweza kupata mafanikio licha ya kushindwa kutwaa mataji.

Mtandao wa Klabu ya Anzhi umekubali uamuzi wa Hiddink kusitisha mkataba wake na kushukuru kutokana na mchango wake ambao ameutoa kwa Klabu hiyo kwa kipindi chote ambacho ameitumikia.

Klabu ya Anzhi imemtakiwa kila la kheri Hiddink katika maisha yake ya baadaye na kutambua kazi ambayo ameifanya na hivyo aendelee na maisha yake mema ya baadaye nje ya Timu hiyo.

Kocha ambaye amekabidhiwa jukumu la kuinoa Anzhi Meulensteen alijiunga na timu hiyo mwezi uliopita na kuanza kufanyakazi pamoja na Hiddink baada ya kukataa ofa ya kuwa chini ya David Moyes.