SOKA-BARCELONA

Klabu ya Barcelona imemtangaza Gerardo Martino kuwa Kocha Mkuu akichukua nafasi ya Tito Vilanova kuinoa Timu hiyo

Gerardo Martin ndiye Kocha Mkuu wa Barcelona anayerithi nafasi ya Tito Vilanova
Gerardo Martin ndiye Kocha Mkuu wa Barcelona anayerithi nafasi ya Tito Vilanova

Mabingwa wa Ligi Kuu nchini Uhispania wamemtangaza Kocha mpya ambaye amekuwa rasmi mrithi wa nafasi ya Tito Vilanova aliyelazimika kuachia wadhifa wake kutokana na kukabiliwa na maradhi ya saratani ya koo. Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Barcelona zimethibitisha timu hiyo imeingia makubaliano na Gerardo Martino raia wa Argentina anayechukua nafasi ya Vilanova na wameshaingia naye mkataba wa miaka mitatu kuinoa timu hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Martino maarufu kwa jina la Tata alishakubaliana masuala yote muhimu na Viongozi wa Barcelona hiyo jana kabla ya leo kutangazwa rasmi kuanza kutekeleza majukumu ya kuwanoa Mabingwa hao La Liga waliopo ziarani nchini Ujerumani.

Mapema kabla ya kutangazwa kushika wadhifa huo wa kuinoa Barcelona Kocha Martino alishaweka bayana benchi lake la ufundi litakuwa pamoja na wasaidizi wake waliokuwa wanakikoa kikosi cha Newell's Old Boys ambao ni Elvio Paolorroso na Jorge Pautasso.

Martino anachukua jukumu la kuifundisha Barcelona huku hakiwa hana rekodi ya kuifundisha Klabu yoyote Barani Ulaya kwani hapo kabla alikuwa anatambulika vizuri kutokana na kufanyakazi hiyo katika Timu ya Argentina pamoja na kuinoa Timu ya Taifa ya Paraguay.

Tata anatajwa kuwa rafiki mkubwa wa baba yake mchezaji bora wa Dunia Lionel Messi, Jorge na taarifa zinadokeza mchezaji huyo amekuwa na ushawishi mkubwa katika kufanikisha kupewa kibarua kwa Kocha huyo.

Uteuzi wake unakuja kipindi hiki ambapo Barcelona imeelekea nchini Ujerumani kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi na kwa sasa ipo chini ya Kocha Msaidizi Rubi.

Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Barcelona zinaeleza kuwa Martino anatarajiwa kuanza kazi yake ya kuifundisha timu hiyo siku ya alhamisi ikiwa ni muda mchache baada ya kutangazwa rasmi kuwa Kocha Mkuu wa Timu hiyo.

Miongoni mwa makocha waliokuwa wanapigiwa upatu kuweza kuchukua mikoba ya Vilanova ni pamoja na Luis Enrique, Ernesto Valverde, Marcelo Bielsa, Jupp Heynckes, Michael Laudrup na Oscar Garcia.

Vilanova alitangaza kwamba kutokana na maradhi ya saratani ya koo yanayomkabili na ushauri aliyopewa na madaktari asingeweza kuendelea kuitumikia timu hiyo ipasavyo na hivyo akafikia uamuzi wa kukaa kando.