SOKA-CHAN

Timu ya Taifa ya Tanzania kutua Uganda kwa ajili ya mchezo wa marudiano kusaka tiketi ya kufuzu CHAN mwakani Afrika Kusini

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania John Bocco akitafuta mbinu za kumpita Beki wa Uganda
Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania John Bocco akitafuta mbinu za kumpita Beki wa Uganda

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kitakwea pipa kueleka nchini Uganda kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wa marudiano dhidi ya Cranes kusaka tiketi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN. Taifa Stars itaelekea nchini Uganda huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa kwa goli 1-0 kwenye mchezo wa awali uliopigwa Jijini Dar Es Salaam na hivyo wanalazimika kushinda mchezo huo ili kuweza kufuzu kwa Fainali za CHAN.

Matangazo ya kibiashara

Timu ya Taifa ya Tanzania inapaswa kushinda si chini ya magoli mawili ili iweze kufuzu kwa Fainali za CHAN ambazo zitafanyika nchini Afrika Kusini hapo mwakani na kushirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen amesema Kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano na wamejiandaa vyema kabisa kuweza kupata ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa siku ya jumamosi.

Kikosi hicho kinachonolewa na Poulsen kilikuwa kimepiga kambi Mkoani Mwanza kwa ajili ya maandlizi ya mchezo huo wa marudiano ambao umepangwa kuchezwa katika Dimba la Namboole.

Poulsen amesema wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo huo na hakuna majeruhi kitu ambacho kinamuongezea imani ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa marudiano na hivyo kuibuka na ushindi.

Kocha huyo ameweka bayana wachezaji wote wanaari ya ushindi na wameshasahau matokeo ya mchezo wa kwanza ambayo yalikuwa ni ya kupoteza mchezo na hivyo sasa wanahitaji ushindi kwa udi na uvumba.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF Boniface Wambura ameshawasiliana na Shirikisho la Soka nchini Uganda FUFA ya kwamba timu hiyo itawasili katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe tayari kwa mchezo huo.

Uganda inaongoza mbele ya Tanzania baada ya kushinda mchezo wa kwanza uliochezwa Jijini Dar Es Salaam baada ya kupata ushindi wa goli 1-0 lililofungwa na Denis Guma katika kipindi cha pili.