SOKA

Kocha wa Manchester United David Moyes asema Wayne Rooney atajunga na Kikosi chake huko Sweden kwa maandalizi ya mwanzoni mwa msimu

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney akishangilia goli dhidi ya Liverpool
Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney akishangilia goli dhidi ya Liverpool Shaun Botterill/Getty Images

Kocha Mkuu wa Klabu ya Manchester United David Moyes amesema anatarajia Mshambuliaji wa Timu hiyo Wayne Rooney ataungana na Kikosi chake kilichopo kwenye michezo ya maandalizi ya msimu ujao.

Matangazo ya kibiashara

Moyes ameweka bayana Rooney ambaye alirudishwa nchini Uingereza kutokana na kukabiliwa na majeraha anatarajiwa kucheza katika mchezo dhidi ya Klabu kutoka Sweden ya AIK Fotboll utakaopigwa tarehe 6 mwezi Agosti.

Rooney mwenye umri wa miaka 27 amekuwa kwenye hali ya kutokuelewana na Moyes ambaye aliweka bayana mshambuliaji huyo ni chaguo la pili kwenye kikosi chake nyuma ya Robin Van Persie.

Mshambuliaji huyo alipata majeraha kwenye mguu wake akiwa nchini Thailand na Kikosi cha Manchester United kilichokuwa kwenye ziara yake ya maandalizi ya msimu mpya na hivyo kurudishwa nyumbani.

Moyes amesema wakati wakatapowasili nchini Sweden basi ana uhakika Rooney ataungana nao katika Jiji la Stockholm kuendelea na michezo ya mwishoni ya maandalizi ya msimu kabla ya kurejea nchini Uingereza.

Kocha huyo ameendelea kusisitiza Rooney hatouzwa licha ya kwamba atakuwa chaguo lake la pili nyuma ya Van Persie amesema Mshambuliaji huyo ameshaanza mazoezi mepesi ikiwa ni ishara ya kupona kwake.

Moyes ambaye timu yake ilipata kichapo kutoka kwa Yokohama Marinos cha magoli 3-2 nchini Japan siku ya jumanne amesisitiza Rooney yupo kwenye mipango yake ya baadaye na hatouzwa kama uvumi unavyoeleza.

Rooney amekuwa akiwindwa na Klabu za Chelsea na Arsenal tangu kuzuka kwa uzushi ameandika barua ya kutaka kuihama Manchester United taarifa ambazo zilikuja kukanushwa baadaye na Uongozi wa timu hiyo.