SOKA

Kocha wa Tottenham Hotspur Villas-Boas ameendelea kusisitiza hawapo tayari kumuuza Mshambuliaji wao Gareth Bale

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Wales na Klabu ya Tottenham Hotspur Gareth Bale anayesakwa na Real Madrid
Mshambuliaji wa Kimataifa wa Wales na Klabu ya Tottenham Hotspur Gareth Bale anayesakwa na Real Madrid

Kocha Mkuu wa Klabu ya Tottenham Hotspur Andre Villas-Boas ameweka bayana dhamira yake ya kutaka kumbakiza Gareth Bale licha ya uwepo wa taarifa za kuendelea kusakwa na Real Madrid.

Matangazo ya kibiashara

Villas-Boas amesisitiza Timu yake haiwezi kumuuza mshambuliaji wake Bale kwa kuwa bado yupo kwenye mipango yao ya baadaye licha ya kwamba ameendelea kuwindwa kwa udi na uvumba na miamba hiyo ya Uhispania Real Madrid.

Kauli ya Villas-Boas imekuja kutokana na uwepo wa taarifa zilizoandikwa kwenye gazeti la Marca la nchini Uhispania likielezea Real Madrid ipo katika hatua za mwisho kuingia mkataba wa miaka sita na Bale.

Kocha huyo amesema Bale ni mchezaji halali wa Tottenham na hawana mpango wa aina yoyote ile ya kumuuza licha ya kwamba kumekuwa na uzushi mwisngi unaomhusu ukieleza amekuwa njia kuondoka White Hart Lane.

Villas-Boas amewaambia wanahabari Bale kwa sasa ni mchezaji ambaye yupo kwenye kiwango cha hali ya juu Duniani na hivyo hawawezi kumpoteza kwani bado yupo kwenye mipango yao.

Bale ambaye alifunga magoli 26 msimu uliopita amekuwa kwenye kiwango bora zaidi tangu amejiunga na Klabu hiyo kitu ambacho kimechangia timu kadhaa kuendelea kummezea mate.

Mshambuliaji huyo alifanikiwa kuzoa tuzo mbili msimu uliopita ikiwemo Mchezaji Bora wa Mwaka pamoja na Mchezaji Bora Chipukizi lakini kwa sasa amekuwa nje ya uwanja akikabiliwa na majeraha.

Kocha Villas-Boas amesema watamkosa Bale kwenye mchezo wa maandalizi ya msimu dhidi ya Sunderland lakini wanaimani katika michezo ijayo ayaendelea kuwepo katika kikosi chao.

Tottenham Hotspur ipo huko Hong Kong kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Asia ambao wanatarajiwa kucheza na Sunderland, Manchester City na kikosi cha Kutoka nchini China ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao.