SOKA

Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard asisitiza Luis Suarez bado anahitajika kuendelea kuwatumikia Vijogoo Vya Jiji

Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard akiwa na Mshambuliaji wa Klabu hiyo Luis Suarez
Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard akiwa na Mshambuliaji wa Klabu hiyo Luis Suarez

Nahodha wa Timu ya Taifa ya Uingereza na Klabu ya Liverpool Steven Gerrard ameainisha harakati zake za kuendelea kufanyakazi kwa nguvu zake zote kuhakikisha Mshambuliaji wao Luis Suarez anaendelea kusalia msimu ujao huko Anfield. Gerrard amesema kwa sasa amekuwa akiendelea kufanya ushawishi wa hali ya juu kumshinikiza Suarez aendelee kusalia na kuchana na mpango wake wakuipa kisogo timu hiyo msimu huu. Suarez anaendelea kuwindwa kwa udi na uvumba na Klabu ya Arsenal ambayo imetoa ofa ya pauni milioni arobaini iliyokataliwa kwa mara nyingine na Liverpool iliyodai mchezaji huyo hauzwi.

Matangazo ya kibiashara

Gerrard amesisitiza Suarez bado ni mchezaji wa Liverpool na wangependa kumuona akiendelea kuwepo kwenye kikosi hicho msimu ujao licha ya mwenyewe kuonesha nia ya kutaka kyondoka Anfield.

Suarez kwa sasa yupo na Kikosi cha Liverpool kilichopo nchini Australia kwa maandilizi ya msimu ujao na tayari Kocha Mkuu Brendan Rodgers amesisitiza mchezaji huyo hatouzwa kwa sasa yupo kwenye mipango yake.

Maneno yake yameendelea kupata nguvu kutoka kwa Mmiliki wa Liverpool John Henry aliyesema licha ya kuitupa ofa ya Arsenal amesisitiza kwamba wao wataendelea kumbakisha mchezaji huyo.

Gerrard kwa upande wake amemsifu Suarez ambaye amemtaja kama miongoni mwa wachezaji wenye kipaji cha kipekee na hivyo anapaswa kuendelea kusalia Anfield kwa muda mrefu zaidi.

Suarez alitangaza nia yake ni kujiunga na Klabu inayocheza Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu huu huku pia akikiri waandishi wa habari wa nchini Uingereza wamechangia maisha yake kuwa magumu.