SOKA

Bayern Munich yaichakaza Barcelona kwa magoli 2-0 kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa Allianz Arena

Mshambuliaji wa Bayern Munich Franck Ribery akikabiliana na beki wa Barcelona kwenye mchezo wa kirafiki
Mshambuliaji wa Bayern Munich Franck Ribery akikabiliana na beki wa Barcelona kwenye mchezo wa kirafiki

Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na Mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ujerumani Bungesliga Klabu ya Bayern Munich imeendeleza ubabe wake dhidi ya Mabingwa wa Ligi Kuu nchini Uhispania La Liga Barcelona na kuwafunga kwenye mchezo wa kirafiki.

Matangazo ya kibiashara

Bayern Munich inayonolewa na Kocha wa zamani wa Barcelona Pep Guardiola imefanikiwa kuibuka na ushindi wa magoli 2-0 kwenye mchezo huo wa maandalizi ya msimu ujao mchezo uliopigwa kwenye Dimba la Allianz Arena.

Magoli ya Bayern Munich kwenye mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Barcelona yaliwekwa kimiani kupitia Nahodha wao Philipp Lahm kabla ya Mshambuliaji Mario Mandzukic aliyeingia akitokea benchi kufunga goli la pili katika kipindi cha pili cha mchezo huo.

Mandzukic alifunga goli hilo zikiwa zimesalia dakika tatu kabla ya mchezo kwisha na kulizamisha kabisa jahazi la Barcelona lililokuwa linaongozwa na Mchezaji Bora wa Dunia Lionel Messi.

Huo ulikuwa mchezo wa tisa wa kirafiki kwa Bayern Munich chini ya Guardiola na kwenye michezo yote imekuwa ikitoka vipigo vikubwa ikiwemo ushindi wa magoli 15-1 dhidi ya Bayern Fanclub Wildenau na kisha kuwafunga Paulaner Dream Team kwa magoli 13-0.

Kipigo hicho kwa Barcelona kutoka kwa Bayern Munich kimekumbusha kichapom walichokipata kwenye hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ambapo waliondolewa kwa jumla ya magoli 7-0.

Kocha Mkuu wa Bayern Munich baada ya mchezo huo amesema kwake ulikuwa mchezo maalum sana kwa sababu katika maisha yake yote amekuwa mchezaji na kocha wa Barcelona hivyo ilikuwa ni siku ya kipekee.

Guardiola amewaambia wanahabari furaha aliyonayo haiwezi kufananisha na kitu chochote kile na anajiona mtu mwenye furaha sana kuiongoza Bayern Munich kupata ushindi dhidi ya Barcelona.

Kikosi cha Bayern Munich kilianza bila ya kuwa na wachezaji wake waliozoeleka akiwemo Franck Ribery, Arjen Robben na Thomas Mueller ambao wamekuwa nguzo imara ya timu hiyo kwa msimu uliopita.

Timu ya Barcelona kwenye mchezo huo ilikuwa chini ya Kocha Msaidizi Jordi Roura na hakikuwajumuisha wachezaji wake mahiri akiwemo Xavi Hernandez, Andres Iniesta pamoja na mchezaji aliyesajiliwa msimu huu Neymar da Silva Santos Júnior.