SOKA

Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers amtaka Luis Suarez kutambua mchango wa mashabiki waliokuwa wanamuunga mkono

Kocha Mkuu wa Liverpool Brendan Rodgers akiwa na mshambuliaji wake Luis Suarez
Kocha Mkuu wa Liverpool Brendan Rodgers akiwa na mshambuliaji wake Luis Suarez

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uruguay anayekipiga katika Klabu ya Liverpool Luis Suarez ameendelea kusumbua vichwa vya wadau wa timu hiyo kipindi hiki kukiwa na taarifa za kuruhusiwa kufanya mazungumzo na Arsenal iliyotangaza utayari wake wa kutoa kitita cha pauni milioni 40 na nyongeza ya pauni moja. Kocha Mkuu wa Liverpool Brendan Rodgers ameendelea kusisitiza hadi sasa Arsenal haijafikia thamani inayostahili kuuzwa kwa mshambuliaji huyo ambaye ameshapewa ruhusa na mmiliki John Henry kuzungumza na The Gunners.

Matangazo ya kibiashara

Suarez anaruhusiwa kuzungumza na Klabu yoyote inayoonesha nia ya kutaka kumsajili iwapo itakuwa tayari kutoa kitita cha pauni milioni zaidi ya arobaini kwa mujibu wa mkataba wake kitu ambacho kimechangia kupewa nafasi hiyo kuzungumza na Arsenal.

Rodgers ameonekana kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Suarez anaendelea kusalia katika Klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao lakini kikwazo kinaweza kuwa ni kwa timu hiyo kutoshiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Kocha huyo wa Vijogoo vya Jiji amemtaka Suarez kuthamini hata mchango wa mashabiki ambao walikuwa naye hata pale alipokuwa na matatizo ikiwemo la kutuhumiwa kwa ubaguzi wa rangi.

Rodgers amemtaka Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uruguay kujali thamani ya mashabiki wa Anfield ambao wameonesha kumpenda licha ya kwamba kuna wakati aliigharimu kutokana na vitendo vyake.

Luis Suarez aliweka bayana nia yake ya kuondoka Liverpool inachangiwa kwa kiasi kikubwa na klabu hiyo kushindwa kucheza Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya wakati yeye nia yake ni kushiriki mashindano hayo.