SOKA

Timu ya Taifa ya Wanawake ya Ujerumani imetinga Fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya kwa kuwafunga Sweden

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Ujerumani wakishangilia ushindi wao dhidi ya Sweden
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Ujerumani wakishangilia ushindi wao dhidi ya Sweden

Timu ya taifa ya Wanawake ya Ujerumani imefanikiwa kutinga hatua ya Fainali ya Mashindano ya Kombe la Ulaya baada ya kuwafunga Sweden kwenye mchezo wa Nusu Fainali.

Matangazo ya kibiashara

Ujerumani imetinga hatua ya Fainali ya mashindano ya Kombe la Ulaya kwa upande wa Wanawake baada ya kupata ushindi wa goli 1-0 katika mchezo uliokuwa mkali kutokana na kila upande kuwa imara.

Goli la pekee la Ujerumani lilifungwa na Dzsenifer Marozsan aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Anja Mittag na yeye kuwazidi ujanja mabenki wa Sweden na hatimaye kuukwamisha mpira huo nyavuni.

Ujerumani imefanikiwa kutinga kwenye hatua ya Fainali ya Kombe la Ulaya upande wa Wanawake kwa mara ya sita mfululizo huku wakiendelea kupigiwa upatu huenda wakaibuka na ubingwa kwa mara nyingine.

Timu ya taifa ya Sweden ilisawazisha goli hilo kupitia kwa Lotta Schelin lakini kwa mshangao wa wengi mwamuzi msaidizi alilikataa goli hilo akisema kuna makosa yalitendeka.

Sweden iliendelea kukutwa na jinamizi la kukosa magoli kwenye mchezo huo huku Ujerumani ikiokolewa mara kadhaa kwa mipira mingi kugonga mwamba na kichwa kuokolewa na mabeki wa timu hiyo.

Ujerumani inasubiri kujua itacheza fainali ya mwaka huu na timu gani kwani baadaye hii kutakuwa na mchezo wa Nusu Fainali ya pili kati ya Norway na Denmark mchezo unaotarajiwa kuwa wa vuta nikuvute.

Ujerumani imetwaa mataji matano yaliyopita na wengi wanataka kuona iwapo itafanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara ya sita kutokana na kushinda fainali zote zilizopita tangu ifungwe na Norway mwaka 1993.