SOKA

Mchezaji wa zamani wa Birmingham, Christian Benitez afariki dunia

REUTERS/Gary Granja

Mshambuliaji wa Ecuador Christian Benitez amefariki dunia nchini Qatar siku ya jumatatu akiwa na umri wa miaka 27. Shirikisho la soka nchini Ecuador limethibitisha taarifa hiyo na kusema mchezaji huyo amefariki kutokana na maradhi ya shinikizo la moyo.

Matangazo ya kibiashara

Kituo cha televisheni cha Gama cha nchini Equador, kimeripoti kuwa Benitez maarufu kwa jina la “Chucho” alifikishwa hospitalini siku ya jumapili akikabiliwa na maumivu ya tumbo na amefariki ghafla siku ya jumatatu baada ya kupatwa na matatizo ya moyo.

Kifo hicho kimewashtua wanachama wa klabu ya El-Jash ya Qatar aliyokaa nayo kwa kipindi kifupi, Benitez alisajiliwa klabuni hapo Julai 6 mwaka huu na siku moja kabla ya kifo chake alishuka dimbani na klabu hiyo iliyokuwa ikimenyana na Qatar Sports Club.

Klabu hiyo imetuma salamu za rambirambi kwa familia na mashabiki wa mchezaji huyo na kusema Benitez hakuwa na matatizo yoyote ya kiafya katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya kwanza toka alipojiunga nayo.

Benitez alijipatia jumla ya mabao manne katika jumla ya michezo 36 aliyoshuka dimbani na kujipatia umaarufu katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.