SOKA-CAF

Al Ahly ya Misri na Orlando ya Afrika Kusini kumenyana mwishoni mwa juma hili

Mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa barani Afrika CAF, Al Ahly ya nchini Misri wametangaza kuwa mechi yao ya kuwania ubingwa wa msimu huu dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliyopangwa kufanyika mwishoni mwa juma hili itapigwa siku ya jumapili katika jiji la El Gouna.

Matangazo ya kibiashara

Awali mechi hiyo ilipangwa kufanyika jijini Cairo lakini wizara ya mambo ya ndani ilizuia kutokana na hofu ya usalama inayochangiwa na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.

Baada makataa hayo, CAF iliipa Al Ahly saa 48 kutafuta sehemu nyingine watakapoweza kufanyia mechi hiyo.

Awali Al Ahly waliwasilisha ombi kwa Shirikisho la Soka la Afrika CAF kuomba mechi hiyo isogezwe hadi Agosti 9 wakati wachezaji wao watakapokuwa wamemaliza mfungo wa Ramadhani lakini ombi hilo lilikataliwa.

Mechi ya kwanza katika hatua ya makundi kati ya Al Ahly na Zamalek ilipigwa nchini humo na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Orlando wanatarajiwa kuwasili jijini Cairo siku ya ijumaa baada ya CAF kukubali mabadiliko hayo.

Nahodha wa Orlando Lucky Lekgwathi amejigamba kuibuka na ushindi kutokana na kufanya maandalizi ya kutosha.