KENYA

Uhaba wa mafuta waichelewesha timu ya riadha ya Kenya kwenye mashindano ya dunia jijini Moscow

Timu ya riadha ya Kenya
Timu ya riadha ya Kenya kenyapage.net

Timu ya riadha ya Kenya imechelewa katika safari yake kuelekea kwenye mashindano ya mabingwa wa dunia jijini Moscow nchini Urusi baada ya kukwama katika uwanja wa ndege wa Kimataifa nchini humo jana Jumatatu kutokana na upungufu wa mafuta uwanjani hapo. 

Matangazo ya kibiashara

Timu hiyo imara ya wanariadha 49 ni miongoni mwa wasafiri 2000 walioathiriwa na upungufu wa mafuta katika uwanja huo, maafisa wamebainisha.
Afisa mmoja katika uwanja huo wa ndege amesema kuwa safari 67 zimeahirishwa ama kucheleweshwa kufuatia msukumo mdogo ambao umesababisha usambaaji wa mafuta kushindikana.

Uwanja huo wa ndege ambao unatumiwa na wakazi wa Afrika Mashariki na Kati, ulifungwa kwa saa kadhaa jana Jumatatu na abiria wapatao elfu moja waliwekwa katika hoteli za kawaida.

Kwa sasa Shughuli za kawaida zimeanza tena katika uwanja huo na timu ya Kenya imeondoka leo asubuhi.

Hata hivyo msemaji wa timu ya riadha Kenya Evans Bosire amesema kuwa ucheleweshwaji huo unaweza kuathiri maandalizi ya timu hiyo kutokana na kwamba imesaliwa na siku mbili pekee za kujiandaa baada ya kuwasili Moscow ambapo mashindano yataanza Agosti 10.

Kenya ilishinda medali saba za dhahabu katika michuano ya mwisho ya Dunia miaka miwili iliyopita huko Daegu, Korea ya Kusini, na kuibuka ya tatu katika jumla ya medali zote.