USAJILI ULAYA- MPIRA WA MIGUU

Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers amwagiza Suarez kufanya mazoezi peke yake

Kocha wa Liverpool, Branden Rodgers akiwa na Luis Suarez
Kocha wa Liverpool, Branden Rodgers akiwa na Luis Suarez Reuters

Uongozi wa klabu ya Liverpool ya nchini Uingereza umemtaka mshambuliaji wake raia wa Uruguay, Luis Suarez kufanya mazoezi akiwa peke yake kutokana na mzozo unaoendelea kati yake na uongozi.

Matangazo ya kibiashara

Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers amesema kuwa amefikia uamuzi huo kutokana na kauli aliyoitoa Suarez juma hili kuwa anashangazwa na hatua ya klabu yake kukataa kumuuza ili ajiunge na klabu ya Arsenal.

Kocha Rodgers pia amekanusha kuwa mchezaji huyo kwenye mkataba wake kulikuwa na kipengele kinachoitaka timu hiyo kumuuza Suarez kwa klabu yoyote inayomtaka kwakuwa eti waliahidiana kuwa wangemuuza iwapo wangeshindwa kutinga kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya mwaka huu.

Taarifa za ndani toka kwa watu wa karibu wa mchezaji huyo zinasema kuwa huenda akawasilisha rasmi maombi yake kwa uongozi kutaka auzwe.

Mashabiki wa Liverpool wameonesha kukasirishwa na kauli za mchezaji huyo ambaye ameendelea kusisitiza kutaka kuihama klabu hiyo kwa kile anachodai imeshindwa kufuzu kwenye hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Arsenal imeonesha nia ya kutaka kumsajili mchezaji huyo lakini wamegonga ukuta kutokana na klabu yake kusisitiza kutotaka kumuuza kwa wakati huu.