LIVERPOOL-SUAREZ

Mmiliki wa klabu ya Liverpool asisitiza kutomuuza mshambuliaji wake Luis Suarez

Mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez.
Mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez. REUTERS/Phil Noble

Mmiliki wa klabu ya vijogoo vya jiji Liverpool, John Henry amesisitiza kuwa mshambuliaji wake raia wa Uruguay Luis Suarez hatouzwa wakati wowote hata baada ya kumalizika kwa dirisha dogo la usajili.

Matangazo ya kibiashara

Henry amesema kuwa klabu yake bado inahitaji huduma za Suarez na hivyo haoni sababu ya kumuuza kwa klabu yoyote kwasasa hata kama fedha itakayowekwa mezani na klabu husika ni ya kiwango cha juu.

Kauli ya mmiliki wa Liverpool inakuja ikiwa imepita siku moja toka kocha wa timu hiyo Brendan Rodgers amwagize Luis Suarez afanye mazoezi mwenyewe kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni kuwa klabu hiyo imekiuka mkataba.

Juma hili mshambuliaji huyo alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachosema kuwa atauzwa iwapo Liverpool imeshindwa kufuzu hatua ya klabu bingwa barani Ulaya, kauli ambayo ilikanushwa vikali na kocha Rodgers.

Luis Suarez ambaye sasa ana umri wa miaka 26 anahusishwa kutaka kujiunga na klabu ya Arsenal ambayo tayari iliweka nia yake ya wazi kumtaka mshambuliaji huyo na kutangaza dau la paundi milioni 30, dau ambalo hata hivyo lilikataliwa.

Licha ya kukataliwa hapo awali, Arsenal kaongeza dau hadi kufikia paundi milioni 40 fedha ambazo safari hii mmiliki wa Liverpool amepigilia msumari akisisitiza mchezaji huyo kutouzwa kwa dau lolote.