UEFA

UEFA yatoa ratiba ya mechi za awali kufuzu kucheza fainali za klabu bingwa barani Ulaya

Ratiba ya michuano ya awali kufuzu kucheza fainali za klabu bingwa barani Ulaya
Ratiba ya michuano ya awali kufuzu kucheza fainali za klabu bingwa barani Ulaya UEFA.com

Shirikisho la kabumbu barani Ulaya UEFA limetoa ratiba ya mechi za awali za kuwania kufuzu kukata tiketi ya kushiriki kwenye hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya, maarufu kama Champions League.

Matangazo ya kibiashara

Ratiba hiyo ambayo imetangazwa hii leo itakuwa katika mfumo wa makundi mawili yaani kwa mfumo wa ligi na ule wa mabingwa.

Katika zile mechi za kuwania kufuzu kukata tiketi ya kucheza klabu bingwa kupitia ligi utazikutanisha klabu za Olympique Lyonnais ya Ufaransa itakayokuwa na kibarua dhidi ya klabu ya Real Sociedad de Fútbol ya nchini Uhispania.

Schalke 04 ya Ujerumani yenyewe itakuwa kwenye kibarua dhidi ya timu ya FC Metalist Kharkiv ya Ukrain, huku klabu ya Paços de Ferreira ya Ureno yenyewe itakuwa na kibarua dhidi ya klabu ya Zenit St Petersburg ya Urusi.

Kwenye mechi nyingine klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi yenyewe itakuwa na kibarua dhidi ya labu ya AC Milan ya nchini Italia wakati klabu ya Fenerbahçe SK ya Uturuki yenyewe itakuwa mwenyeji wa klabu ya Arsenal FC ya nchini Uingereza.

Kwenye hatua ya mabingwa klabu ya GNK Dinamo Zagreb ya Croatia yenyewe itawakaribisha timu ya FK Austria Wien ya Austria huku klabu ya PFC Ludogorets Razgrad ya Bulgaria itakuwa mwenyeji wa timu ya FC Basel 1893 ya Uswis.

Kwenye mtanange mwingine klabu ya Viktoria Plzeň ya Jamhuri ya Czech itakuwa mwenyeji wa timu ya NK Maribor ya Uslovania wakati timu ya Shakhter Karagandy ya Kazakistan itakuwa mwenyeji wa klabu ya Celtic FC ya Uscotish, huku kwenye mtanange mwingine klabu ya Steaua Bucureşti Romania itakuwa wenyeji wa klabu ya  Legia Warszawa ya Poland.

Katika hatua nyingine ushiriki wa timu za Fenerbahçe SK na FC Metalist Kharkiv kwenye hatua hii ya kukata tiketi ya kufuzu utaendelea kuwepo wakati wakisubiri uamuzi wa kamati ya nidhamu ya UEFA.