SOKA-CHAN

Zimbabwe yaifunga Zambia na kufuzu michuano ya CHAN

Timu ya taifa ya soka ya Zimbabwe imefuzu katika fainali ya michuano ya bara Afrika CHAN inayowashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani.

Matangazo ya kibiashara

Zimbabwe iliifunga Zambia bao 1 kwa 0 na kujikatia tiketi ya kwenda Afrika Kusini baada ya kuwaangusha wenyeji wao katika uwanja wao wa nyumbani wa Levy Mwanawasa mjini Ndola.

The Warriors wanafuzu kutokana na bao hilo la ugenini na pia kwa kulazimisha sare ya kutofungana na Zambia mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Harare.

Charles Sibanda ndiye aliyeipa timu yake ushindi katika dakika ya 65 ya mchuano huo ambao wengi walitarajia kuwa Zambia wangeshinda na kufuzu katika fainali hizo.

Tayari mataifa mengine kama Burkina Faso, Burundi, Congo Brazzaville, Ethiopia, Gabon, Ghana, Libya, Mali, Mauritania, Morocco, Nigeria na Uganda yamefuzu katika michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi kati ya tarehe 11 Mwezi Januari na tarehe 1 mwezi Februari mwaka ujao.

Wachambuzi wa soka nchini Zambia wanasema kuwa hatima ya kocha wa Chipolopolo Mfaransa Harve Renard kuendelea kuwa mkufunzi wa kikosi hicho katika siku zijazo huenda ikaanza kuyumba baada ya kushindwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Renard aliiongoza Zambia kunyakua kwa mara ya kwanza taji la timu bora barani Afrika mwaka uliopita nchini Gabon na Equitorial Guinea na kushindwa kulitetea nchini Afrika Kusini mapema  mwaka huu.

Mbali na michuano ya CHAN , Chipolopolo inajiandaa kumenyana na Black Stars ya Ghana katika mchuano wa kusaka tiketi ya kufuzu katika mzunguko wa mwisho wa kutafuta nafasi ya kucheza katika kombe la dunia nchini Brazil  mwaka ujao.

Zambia wanahitaji ushindi ili kusonga mbele kwa sababu wana alama 11 huku wapinzani wao Ghana wao wanahitaji tu sare ili kufuzu kwa sababu wanaongoza kundi lao kwa alama 12.