CAF

CAF yaamua mechi za klabu bingwa kuchezwa Misri

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limetangaza kuwa mechi mbili za kundi la A kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika zitachezwa nchini Misri mwishoni mwa juma hili.

Matangazo ya kibiashara

CAF ambayo makao yake ni jijini Cairo imefikia uamuzi huo licha ya kuwepo kwa hali ya wasiwasi kuhusu usalama katika nchi hiyo ambayo imekuwa ikikumbwa na maandamano ya kisiasa.

Al Ahly watamenyana na watani wao wa jadi Zamalek FC, huku mchuano mwingine ukiwa kati ya AC Leopards ya Congo dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika mji wa El Gouna.

Vlabu vyote vya Misri vipo katika kundi moja, kundi ambalo Orlando Pirates wanaongoza kwa alama saba mbele ya Al Ahly ambayo  ina alama nne sawa na Leopard huku Zamalek ikiwa ya mwisho kwa alama moja.

Kocha wa Al Ahly Mohamed Youssef amesema kuwa amesikitishwa na uamuzi huo wa CAF ambao anasema utaathiri sana wachezaji wake kwa sababu ya hali mbaya ya uwanja mjini El Gouna na joto jingi.

CAF imesema kuwa mechi hizo mbili hazitahudhuriwa na mashabiki kwa sababu za kiusalama na zitachezwa kuanzia saa kumi jioni saa za Cairo.

Kutokana na ongezeko la machafuko nchini Misri kwa kipindi cha miaka miwili sasa ligi kuu ya soka nchini humo imesitishwa na mashabiki hawaruhusiwi kuhudhuria mechi za Kimataifa.

Kundi la B  lina  Esperence ya Tunisia inaongoza kundi hilo likiwa na alama 6 ikifuatwa na Coton FC ya Cameroon  ambayo pia ina alama 6, Sewe FC ya Cote Dvoire na Libolo FC ya Angola zote zina alama tatu.