SOKA

Didier Six akubali kuiongoza Togo kumenyana na DRC mwezi ujao.

Kocha Didier Six raia wa Ufaransa aliyekuwa ametangaza kujiuzulu kuwa Mkufunzi  wa timu ya taifa ya soka ya Togo amekubali kuiongoza timu hiyo katika mchuano wa mwisho wa kufuzu kwa kombe dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi ujao.

Matangazo ya kibiashara

Mwezi Juni, kocha  Six alinukuliwa akisema kuwa alikuwa ametofautiana na viongozi wa shirikisho la soka la Togo kwa kutolipwa marupurupu yake na hivyo hangeweza kuendelea kuifunza timu hiyo.

Mchuano huo wa kundi I hauna uzito wowote kwa timu hizo mbili kwa sababu tayari zilikuwa zimeondolewa katika kinya'nga'nyiro cha kufuzu katika mzunguko wa pili wa kusakata tiketi ya kufuzu kwenda kushiriki katika kombe ka dunia nchini Brazil mwaka ujao.

Chama cha soka nchini Togo kinasema kuwa licha ya timu yao kuondolewa katika safari ya kwenda Brazil,  mchuano wa mwisho na DRC ni muhimu kwa kocha Six ambaye amekuwa kocha wao  kwa miaka miwili.

Hata hivyo, Cameroon na Libya ambazo zipo katika kundi hilo zitakuwa na kazi ngumu mwezi ujao kutafuta nafasi ya kufuzu katika mzunguko wa mwisho kwa sababu Cameroon wanahitaji sare ili kusonga mbele huku Libya wakihitaji ushindi.

Cameroon wanaongoza kundi hilo kwa alama 10 huku Libya ikiwa ya pili kwa alama 9.

Mataifa kumi kutoka barani Afrika yatamenyana katika mzunguko wa mwisho kutafauta mataifa matano yakayokwenda Brazil mwakani.