SOKA

Manchester United yasema haijapanga kumsajili Gareth Bale

Kocha wa klabu ya soka ya Manchester United ya Uingereza David Moyes anasema kuwa klabu yake bado haijatoa kitita chochote cha kumsajili mshambulizi wa Tottenham Hotspurs Gareth Bale.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo Moyes amesema kuwa hawezi kukataa kabisa ikiwa Manchester United itasonga mbele na kumpata Bale ambaye kwa sasa anaelekea kusajiliwa na klabu ya Real Madrid ya Uhispania.

Aidha, Moyes ameongeza kuwa United itaendelea kumsaka mchezaji ambaye ataisaidia timu yake kufanya vizuri katika ligi kuu ya soka nchini Uingereza.

Imekuwa ikiripotiwa kuwa tayari Real Madrid imekubali kutoa kitita cha Pauni Milioni 86 kumsajili Bale kwa kipindi cha miaka sita.

Katika hatua nyingine, kocha wa Chelsea Jose Mourihno baada ya timu yake kulazimisha sare ya kutofungana na Manchester United katika ligi kuu ya soka Jumatatu, amesema kuwa matumaini ya kumsajili mshambulizi wa United Wayne Ronney yameanza kudidimia.

Kocha huyo wa Chelsea sasa anasema kuwa amempa Ronney siku mbili kuamua ikiwa angependa kuichezea Chelsea au kusalia Manchester United klabu ambayo anasema Rooney hajapata uungwaji mkono.

Uongozi wa United umeendelea kusisitiza kuwa hautamuuza Wayne Rooney na tayari Chelsea inasema kuwa ikiwa hali itaendelea kuwa hivyo basi itabidi wamtafute mshambulizi mwingine.

Baada ya mchuano wa siku ya Jumatatu, Chelsea bado wanaongoza msururu wa ligi kwa alama 7 , Liverpool ni ya pili kwa alama sita sawa na Tottenham Hotspurs.

Manchester United inashikilia nafasi ya nne kwa alama nne.