TENNIS

Serena Williams aanza kutetea taji lake katika michuano ya US OPEN

Bingwa mtetezi wa taji la US Open katika mchezo wa Tennis kwa upande wa wanawake Serena Williams ameanza vema juhudi za kutete taji lake aliloshinda mwaka uliopita baada ya kumshinda Francesca Schiavone wa Italia kwa seti za 6-0, 6-1 katika mchuano wa ufunguzi.

Matangazo ya kibiashara

Serena Williams ambaye pia anaorodheswa kuwa mchezaji bora kwa upande wa wanawake duniani, anasaka kuandikisha historia kwa kutafuta  taji lake kuu la 17 na taji la tano la US Open.

Williams amesema amefurahi kuanza kwa ushindi kwa kumwangusha bingwa wa zamani katika mchezo huo ambao ulimalizika muda mfupi kabla ya mvua kubwa kuanza kunyesha.

Ikiwa atafanikiwa kushinda taji la mwaka huu, Williams mwenye umri wa miaka 31 atakuwa mchezaji mkongwe katika historia ya michezo hiyo kuwahi kushiriki na kushinda taji hilo na kushinda kwa upande wa wanawake.

Wachambuzi wa mashindano haya ya US OPEN wanasema kuwa Victoria Azarenka kutoka nchini Belarus anaendelea kutoa ushindani mkubwa kwa Serena hasa baada ya wawili hao kukutana mara mbili mfululizo katika fainali ya mashindano hayo.

Kwa upande wa wanaume, Mhispania Rafael Nadal naye alianza vizuri kwa kumshinda Mmarekani Ryan Harrison kwa seti za 6-4 6-2 6-2.

Nadal anarejea katika mashindano ya US Open baada ya kukaa nje mwaka uliopita kwa sababu ya jeraha la goti na anacheza kwa mara ya kwanza baada ya kumshinda Novak Djokovic mwaka 2011.