FIFA

FIFA yamfungia mchezaji wa Morroco kwa siku 30

DR

Shirikisho la soka duniani FIFA limemfungia mchezaji wa timu ya taifa ya Morroco baada ya kubainika kuwa alitumia dawa iliyopigwa marufuku katika mchezo wa soka.

Matangazo ya kibiashara

FIFA haijamtaja mchezaji huyo lakini imesema imemfungia kwa siku 30 na tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi yake wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza na Cote Dvoire katika mchuano wa mwisho mwezi ujao wa kufuzu kwa kombe la dunia.

Mchezaji huyo alibainika kutumia dawa hiyo inayoaminiwa kusisimua misuli wakati wa mchuano wa kufuzu kwa kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil baada ya kuishinda Gambia mabao 2 kwa 0.

FIFA imempa mchezaji huyo hadi tarehe 4 mwezi wa Septemba ikiwa anataka kusikilizwa na Kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo lakini itabidi mchezaji huyo awasilishe utetezi wake kupinga uamuzi huo wa FIFA tarehe 11 mwezi Septemba.

Mbali na hilo, rais wa shirikisho la soka barani UEFA Michel Platini amesema kuwa hana uhakika ikiwa atawania urais wa FIFA wakati wa uchaguzi mwaka 2015.

Platini ambaye wachambuzi wa soka wanasema kuwa huenda akawa kiongozi wa FIFA katika siku zijazo, amedokeza kuwa atazungumzia uamuzi wake kwa undani wakati wa mkutano wa Kamati ya juu ya UEFA mwezi ujao.

Platini amekuwa akiongoza UEFA tangu mwaka 2007 huku rais wa sasa wa FIFA Sepp Blatter akiwa uongozini tangu 1998.