TENNIS

Venus Williams abanduliwa nje ya michuano ya US Open

Bingwa mara mbili wa michuano ya mchezo wa Tennis ya US Open kwa upande wa akina dada Venus Williams kutoka Marekani ameondolewa katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo baada ya kufungwa na Zheng Jie wa China kwa seti 6-2, 2-6, 7-6 (7-5).

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo ulichezwa kwa muda wa saa 3 na dakika 2 na unaingia katika vitabu vya historia vya mchezo  huo kwa upande wa akina dada kuchezwa kwa muda mrefu tangu mwaka 1970.

Venus amesema kuwa alijaribu kadiri ya uwezo wake kushinda lakini haikuwa rahisi na kuondolewa kwake kunadhihirisha wazi kuwa huu si mwaka wake katika michuano hiyo  na amempongeza mpinzani wake kwa kucheza vizuri.

Aidha, ameongeza kuwa jeraha la mgongoni alililolipata pia limemsababisha kutofanya vizuri katika michuano hiyo ambayo kwa miaka mitatu mfululizo amekuwa akiondolewa katika mashindano hayo.

Venus kwa sasa atasalia tu  kumshabikia dadake Serena Williams ambaye ni bingwa mtetezi wa michuano hii.

Williams ambaye pia anaorodheswa kuwa mchezaji bora kwa upande wa wanawake duniani, anasaka kuandikisha historia kwa kutafuta  taji lake kuu la 17 na taji la tano la US Open.

Ikiwa atafanikiwa kushinda taji la mwaka huu, Williams mwenye umri wa miaka 31 atakuwa mchezaji mkongwe katika historia ya michezo hiyo kuwahi kushiriki na kushinda taji hilo na kushinda kwa upande wa wanawake.

Kwa upande wa wanaume, bingwa mtetezi wa michuano hiyo Andy Murray amefika katika mzunguko wa pili baada ya kumshinda Mfaransa Michael Llodra kwa seti za 6-2 6-4 6-3.

Murray raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 26 sasa atamenyana na Leonardo Mayer kutoka Argentina katika mzungumzo wa pili ya michuano hii.