RIADHA

Usain Bolt ang'ara katika mbio za Diamond League

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 100 Mjamaica Usain Bolt licha ya kuanza kwa kusuasua wakati wa fainali ya mashindano ya Kimataifa ya Diamond League jijini Zurich nchini Ujerumani alifanikiwa kumaliza wa kwanza kwa muda wa sekunde 9 nukta 90.

Matangazo ya kibiashara

Mwanaridha huyo mwenye umri wa miaka 27 alimshinda Mjamaica mwenzake Nickel Ashmeade aliyemaliza kwa muda wa sekunde 9 nukta 94 huku Mmarekani Justin Gatlin akimaliza wa tatu kwa muda wa sekunde 9 nukta 96.

Kabla ya mbio hizo, Bolt alikuwa amedokeza kuwa alitamani kukimbia kwa muda wa sekunde 9 nukta 80 lakini hakufanikiwa kwa sababu alianza vibaya mbio hizo Alhamisi usiku.

Katika mbio za Mita 5,000 kwa upande wa wanawake, ushindani mkali ulikuwa kati ya Waethiopia lakini Meseret Defar alimaliza kwa nguvu na kunyakua ushindi mbele ya mpinzani wake Tirunesh Dibaba.

Defar ambaye ni bingwa wa duniani katika mbizo hizo na pia bingwa wa michezo ya Olimpiki alimaliza wa kwanza kwa muda wa dakika 32 nukta 83 sekunde mbili mbele ya Dibaba huku nafasi ya tatu ikimwendea Mkenya Mercy Cherono.

Bingwa mpya wa dunia katika mita 800 kwa upande wa wanawake Eunice Sum alimaliza wa kwanza katika mbio hizo kwa muda wa dakika 1 nukta 58.

Kenya pia ilifanya vizuri katika mbio za Mita 3,000 kuruka maji na viunzi  kwa upande wa wanaume kwa  kushinda nafasi zote tatu wakiongozwa naConseslus Kipruto, huku bingwa wa dunia katika mbio hizo Ezekiel Kembo akimaliza katika nafasi ya 10.

Mshindi wa kwanza katika mashindano hayo ya riadha hushinda Dola 40,000 za Marekani.