HISPANIA

Gareth Bale atambulishwa rasmi Real Madrid, azoa kitita mamilioni ya euro

REUTERS/Rebecca Naden

Maelfu ya mashabiki wa Real Madrid ya Hispania wamefurika katika uwanja Bernabeu kwa ajili ya kumshuhudia mchezaji Gareth Bale ambaye ametambulishwa rasmi kuchezea timu hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Gareth Bale anajiunga na Real Madrid akitokea Tottenham Hotspur katika mkataba mnono unaoelezewa kuvunja rekodi ya dunia na mchezaji huyo anakua mchezaji namba moja kwa wachezaji wenye gharama zaidi katika usajili wao.

Mchezaji huyo ameingia mkataba wa miaka sita wenye thamani ya kitita cha euro milioni 100 baada ya kukamilka kwa mchakato mrefu wa usajili huo.

Gareth Bale mwenye umri miaka 24 amepokelewa kwa shangwe na mashabiki wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya La Liga waliokua na shauku ya kumuona.

Mchezaji huyo amemwaga wino kutia saini huku rais wa klabu hiyo tajiri Florentino Perez akimtambulisha na kushuhudia utiaji saini huo.

Perez amemtambulisha Gareth Bale mbele ya mashabiki na kueleza kuwa Bale ni mcheazaji wa aina yake na alikua na ndoto za siku nyingi za kuchezea klabu hiyo.

Perez amesema kuwa jitihada za mchezaji Bale ndizo zimemwezesha mchezaji huyo kufika katika klabu hiyo ambazo zimekua ndoto za siku nyingi kwa kinda huyo.

Bale kwa upande wake ameelezea kufurahishwa na mapokezi aliyofanyiwa na uongozi wa klabu hiyo pamoja na mashabiki na kuongeza kuwa ndoto yake sasa imekua kweli baada ya kusaini kukipiga katika klabu ya Real Madrid.

Bale amewafurahi na kuwashitusha mashabiki wake baada ya kutoa hotuba fupi kwa lugha ya kihispania na hivyo kulazimisha mashabiki hao kulipuka wakishangilia.

Kocha wa Real Mdrid Carlo Ancelotti ameonyesha kuwa na matumaini makubwa kutoka kwa mchezaji huyo na anaamini kuwa ujio wake utaisaidia klabu yake kwa kushirikiana na wacheji kama akina Cristiano Ronaldo na Karim Benzema.