GHANA

Ghana yajipanga kutinga fainali za Kombe la Dunia, Michael Essien aanza mazoezi

RFI

Mchezaji wa timu ya taifa ya Ghana ambaye pia ni kiungo wa klabu ya Chelsea ya Uingereza Michael Essien ameanza mazoezi na timu hiyo inayojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka ujao mchezo utakaopigwa ijumaa dhidi ya Zambia.

Matangazo ya kibiashara

Mchezaji huyo ameanza mazoezi na timu hiyo jana ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Michael Essien aliichezea timu yake ya Ghana zaidi ya miaka miwili iliyopita kbla ya kuamua kuelekeza nguvu zaidi katika klabu yake.

Michael Essien mwenye umri wa miaka 30 alifanya uamuzi huo hasa baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maumivu ya goti na sasa ameamua kurejea katika kikosi cha timu ya taifa.

Wachezaji wengine walioshiriki katika mazoezi hayo ni nahodha Asamoah Gyan, Albert Adomah, Rashid Sumaila, Mahatma Otoo, Kwadwo Asamoah, Jonathan Mensah, Razak Braimah, Fatau Dauda, Rabiu Mohammed, Christian Atsu, Mubarak Wakaso na Awal Mohammed.

Wachezaji wengine ambao wanatarajiwa kuwasili leo ni pamoja na Kevin-Prince Boateng kujiunga na wenzao katika maandalizi hayo ambapo timu ya Ghana inahitaji pointi moja tu ili iweze kuingia katika hatua timu kumi ambazo zitachujwa na kubaki tano kwa ajili ya kuwakilisha Bara la Afrika katika fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.