US OPEN 2013

Rafael Nadal atwaa taji lake la pili la michuano ya US Open

Mshindi wa fainali ya michuano ya US Open, Rafael Nadal akibusu kombe alilokabidhiwa usiku wa kuamkia leo
Mshindi wa fainali ya michuano ya US Open, Rafael Nadal akibusu kombe alilokabidhiwa usiku wa kuamkia leo Reuters

Rafael Nadal amefanikiwa kumfunga mchezaji nambari moja wa mchezo wa tenesi duniani Novak Djokovic kwenye fainali ya michuano ya US Open na kufanikiwa kutwaa taji lake la pili la mashindano hayo.

Matangazo ya kibiashara

Nadal mwenye umri wa miaka 27 alionesha umahiri mkubwa wakati wa seti zote nne na kutoa upinzani mkali kwa Djokovic ambaye muda mwingi alionekana kujidhatiti kumdhibiti mpinzani wake.

Kwenye mchezo huo ambao ulidumu kwa zaidi ya saa tatu na dakika 21 ulishuhudia Nadal akichomoza na ushindi wa seti tatu kwa moja kwa matokeo ya 6-2, 3-6, 6-4 na 6-1.

Kwa ushindi huu Nadal sasa atakuwa maejinyakulia mataji 13 ya ubingwa na kuungana na bingwa wa zamani Pete Sampras na Roger Feder mwenye mataji 17 ya ubingwa.

Nadal ambaye alikosa mashindano ya mwaka jana ya US Open kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti hivi sasa anatarajiwa kurejea kwenye nafasi yake ya kwanza kwa ubora wa mchezo huo baada ya ushindi wake wa jana.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ushindi huo, Nadal amesema kuwa hakutarajia kushinda taji hilo na kwamba mpinzani wake Novak djokovic alimpa wakati mgumu kufikia mafanikio.

Kwa upande wake Djokovic amempongeza Nadal kwa kuonesha mchezo mzuri na kukiri kuwa kushindwa kwake kulitokana na makosa ya mara kwa mara aliyokuwa akiyafanya wakati akianzisha mpira kwenda kwa mpinzani wake.