SOKA-ULAYA

Kocha wa Manchester United anahitaji nguvu zaidi ili kuimarisha ngome yake

Reuters/Phil Noble

Meneja wa Manchester United David Moyes amesema anahitaji wachezaji zaidi ili kuimarisha kikosi chake na amewatahadharisha mashabiki kuwa huenda kipigo kama kile cha mabao 4-1 walichopata toka kwa Manchester City mwishoni mwa juma kikajirudia tena wakati mwingine.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na waandishi habari kabla ya pambano la hii leo la kombe la Capital One dhidi ya Liverpool, Moyes aliyechukua mikoba ya Sir Alex Ferguson amesema ni lazima klabu hiyo ikabiliane na changamoto kwa wakati huu kwani ipo katika kipindi cha mpito.

United iliwakosa baadhi ya wachezaji maarufu katika dirisha la usajili msimu huu na Kocha Moyes anaona kuwa bado wana kibarua kigumu cha kuwasaka wachezaji watakaojumuishwa na kikosi hicho na hata wale watakaoweza kuingia moja kwa moja.

Juhudi za United kutaka kuwanasa wanasoka nyota kama Cesc Fabregas wa Barcelona, Ander Herrera wa Athletic Bilbao na Fabio Coentrao wa Real Madrid hazikufua dafu.

Katika dakika za lala salama kabla ya kufungwa dirisha la usajili msimu huu, United ilifanikiwa kumsajili kiungo wa Ubelgiji Marouane Fellaini aliyetokea Everton.

Mashabiki wa klabu hiyo wanasubiri kuona United itaambulia nini katika mechi yake ya hii leo ya kuwania ubingwa wa kombe la Capital One dhidi ya Liverpool.

Michuano mingine itakayotimua vumbi hii leo ni kati ya Newcastle United dhidi ya Leeds, West Bromwich Albion dhidi ya Arsenal, Birmingham dhidi ya Swansea wakati Tranmere wao watachuana na Stoke.