Michezo

Messi afika mahakamani leo Ijumaa kujibu mashtaka ya kukwepa kodi

Mchezaji wa Barcelona  Lionel Messi
Mchezaji wa Barcelona Lionel Messi REUTERS/Albert Gea

Mchezaji wa kimataifa wa klabu ya Barcelona ya Hispania Lionel Messi hii leo amefika katika mahakama kujibu mashitaka ya tuhuma za ukwepaji kodi.

Matangazo ya kibiashara

Messi anakabiliwa na tuhuma za kukwepa kodi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni tano inadhaniwa kuwa inaweza kushusha umaarufu wa mwanadinga huyo bora mara nne wa dunia.

Messi mwenye asili ya Argentina katika kesi hiyo ya ukwepaji kodi inayomhusisha baba yake pia amekataa kuzungumza lolote kabla na baada ya kuanza kusikilizwa kwa kesi yake.

Kesi ya Messi mwenye umri wa miaka 26 imesikilizwa kwa faragha katika mahakama ya Kitongoji cha GAVA mjini Barcelona eneo ambako anaishi na mchezaji huyo ameonekana kujiamini akitaraji kushinda kesi hiyo.

Mwanasheria wa Messi Cristobal Martel amewaaambia waandishi wa habari kuwa mteja wake ana shauku kubwa ya kumaliza shitaka hilo na mamlaka ya kodi badala ya kuendelea kuvutana na serikali ili aweze kuendelea na shughuli zake.

Messi pamoja na baba yake Jorge Messi wamekana tuhuma hizo na kumshushia lawama wakala wa zamani wa mchezaji huyo kwa kutotekeleza wajibu wake katika masuala ya kodi.

Katika hatua nyingine mahakama hiyo imesema kuwa kuna taarifa kuwa Messi pamoja na baba yake Jorge Messi walilipa fedha hizo na malipo ya ziada kama faini mwezi Agosti na hatua hiyo huenda ikapunguza makali ya hukumu kama watakutwa na hatia.