SOKA-ULAYA

Nyota ya Manchester United yazidi kufifia katika msimu huu wa ligi kuu ya Uingereza

REUTERS/Stefan Wermuth

Klabu ya soka ya Manchester United imeendelea kupata machungu katika msimu huu wa ligi kuu ya Uingereza baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 toka kwa West Bromwich Albion kwenye uwanja wa Old Trafford.

Matangazo ya kibiashara

Kichapo cha Man U ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo kinaendeleza rekodi mbaya katika msimu huu ikiwa ni changamoto kubwa kwa kocha David Moyes aliyechukua mikoba ya Sir Alex Ferguson aliyekuwa akiinoa klabu hiyo.

Mabao ya West Brom yalipachikwa nyavuni na Morgan Amalfitano na Saido Berahino, wakati bao moja la kufutia machozi la Man U lilipachikwa na Wayne Rooney.

Manchester City ambao juma lililopita waliwaaibisha mahasimu wao Man U kwa kichapo cha mabao 4-1, nao hawakuwa na siku nzuri baada ya kupata kichapo cha nyumbani magoli 3-2 toka kwa Aston Villa.

Kwa matokeo hayo Man U imeendelea kusalia katika nafasi ya 12 ya msimamo wa ligi, wakati mahasimu wao Man City wakishika nafasi ya 5. Arsenal imeendelea kusalia kileleni ikiwa na alama 15 ikifuatiwa na Tottenham yenye alama 13. Chelsea ni ya 3 ikiwa na alama 11 sawa na Southampton yenye alama 11 katika nafasi ya 4.