SOKA-BARCELONA

Barcelona kukosa huduma ya Lionel Messi kwa kipindi cha majuma matatu baada ya kuumia nyama za paja

Klabu ya Barcelona ya nchini Hispania inatarajiwa kukosa huduma ya Mshambuliaji wake wa Kimataifa wa Argentina na Mchezaji Bora wa Dunia Lionel Messi kwa kipindi cha majuma matatu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.

Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi akishangilia moja ya magoli aliyofunga dhidi ya Ajax
Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi akishangilia moja ya magoli aliyofunga dhidi ya Ajax REUTERS/Albert Gea
Matangazo ya kibiashara

Maumivu ya Messi aliyapata kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Almeria ambapo Barcelona walifanikiwa kupata ushindi wa magoli 2-0 na hivyo kuendelea kujiwekea mazingira mazuri ya kutetea Ubingwa wao msimu huu.

Mshambulizji huo mahiri ameondolewa kwenye kikosi cha Barcelona ambacho kimesafiri kuelekea nchini Scotland kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Celtic utakaopigwa siku ya jumanne.

Messi ambaye ameendeleza rekodi yake nzuri ya ufungaji msimu huu kwa kufunga katika michezo yote saba ya Barcelona anatarajiwa kukosekana kwa majuma matatu kitu ambacho kinaweza kikateteresha safu ya ushambuliaji.

Hii ni mara ya pili kwa Messi kuumia katika msimu huu na hivyo atakosa michezo mwili ya Ligi ya nyumbani ya La Liga dhidi ya Valladolid na Osasuna lakini pia atakosa mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Celtic.

Taarifa iliyotolewa na Klabu imethibitisha Messi amepata majeraha ambayo si makuba sana na hivyo atalazimika kuwa nje kwa majuma matatu ili kuhakikisha anapona ndiyo aweze kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Barcelona imeendelea kuandamwa na zimwi la majeruhi baada ya Javier Mascherano naye kulazimika kukosa safari baada ya kuumia na kuungana na Jordi Alba pamoja na Carles Puyol ambaye amekuwa anasumbuliwa na maumivu kwa muda mrefu.