SOKA-LIVERPOOL

Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers asema washambuliaji wake Suarez na Sturridge ndiyo bora zaidi Uingereza

Kocha Mkuu wa Liverpool Brendan Rodgers ameibuka na kusifu timu yake ndiyo yenye safu hatari zaidi ya ushambuliaji na hili limekuja kutokana na ushindi alioupata kwenye mchezo dhidi ya Sunderland huku washambuliaji wake wawili wakifunga magoli yao matatu. Rodgers amethubutu kutamka hadharani ushirikiano kati ya washambuliaji wake Luis Suarez na Daniel Sturridge ndiyo hatari zaidi kwa sasa na ana uhakika wachezaji hao wawili wataleta mafanikio makubwa sana msimu huu.

Washambuliaji wa Klabu ya Liverpool Daniel Sturridge na Luis Suarez wakishangilia moja kati ya magoli matatu waliyoshinda dhidi ya Sunderland
Washambuliaji wa Klabu ya Liverpool Daniel Sturridge na Luis Suarez wakishangilia moja kati ya magoli matatu waliyoshinda dhidi ya Sunderland
Matangazo ya kibiashara

Suarez alirejea dimbani baada ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa michezo kumi na katika mchezo wa kwanza dhidi ya Manchester United kwenye mashindano ya Capital One hakuweza kufunga ila jana alipachika magoli mawili kati ya matatu.

Liverpool imefanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-1 mbele ya Sunderland huku Suarez akipiga magoli mawili na mwenzake Sturridge akifunga goli moja na kuifanya timu hiyo kuzoa pointi tatu muhimu.

Rodgers amewaambia wanahabari hana uhakikika kama kuna ushirikiano bora zaidi ya washambuliaji wake hao wawili kwenye Ligi Kuu nchin Uingereza na kusema maneno yake yataonekana ya kweli kadri michezo itakavyokua inaendelea.

Liverpool imefanikiwa kurejea kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza nyuma ya vinara Arsenal wakitofautiana kwa pointi mbili baada ya kucheza michezo sita hadi sasa.

Rodgers amekiri amefikia uamuzi wa kusema washambuliaji hao wawili ndiyo bora kwa sasa kutokana na umahiri waliouonesha kwenye mchezo dhidi ya Sunderland na hilo lilionekana kwa kila mtu aliyefuatilia mchezo huo.

Kocha huyo ambaye ameshaondolewa kwenye Kombe la Capital One ameendelea kufarijika na kurejea kwa Suarez anayeonekana kuongeza makali ya safu yake ya ushambuliaji kitu kinachomfanya aamini kutakuwa na mapinduzi kwenye safu yake ya ushambuliaji.