SOKA-GALATASARAY

Roberto Mancini huenda akapewa kibarua cha kuinoa Galatasaray iwapo atakubaliana na Uongozi kwenye mazungumzo yanayoendelea

Kocha wa zamani wa Manchester City Roberto Mancini akiwajibika wakati akiwa na Klabu hiyo
Kocha wa zamani wa Manchester City Roberto Mancini akiwajibika wakati akiwa na Klabu hiyo

Klabu ya Galatasaray ya nchini Uturuki ipo kwenye mazungumzo na Kocha wa zamani wa Manchester City Roberto Mancini kwa lengo la kumpa kibarua cha kukinoa kikosi chao kutokana na Klabu hiyo kumtimua Kocha wake.

Matangazo ya kibiashara

Klabu ya Galatasaray imethibitisha kuanza mazungumzo na Mancini aliyetimuliwa nchini Uingereza baada ya kushindwa kutwaa taji lolote msimu uliopita wa Ligi Kuu na kuambulia kumaliza nafasi ya pili.

Rais wa Klabu ya Galatasaray Unal Aysal pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Lutfi Aribogan wamekutana na Mancini kwa mazungumzo kuangalia iwapo wataafikiana ili aweze kuanza kazi ya kuifundisha timu hiyo.

Galatasaray wamelazimika kuanza kibarua cha kusaka kocha mwingine baada ya kumtimua Fatih Terim juma lililopita ikiwa ni siku chache baada ya kupata kipigo cha mbwa mwizi kutoka kwa Real madrid kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Mancini huenda akachukua nafasi ya Terim aliyefukuzwa baada ya kushindwa kufikia makubaliano na Uongozi wa Galatasaray juu ya kuongeza mkataba wa kuendelea kuifundisha Klabu hiyo.

Terim alikuwa ni mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Klabu ya Galatasaray na amefanikiwa kuipa mataji sita miongoni mwa makombe kumi na kenda ambayo timu hiyo imeshinda kwenye historia yake.

Kocha huyo wa Galatasaray anatimuliwa kipindi hiki timu hiyo ikiwa kwenye nafasi ya kumi kwenye msimamo ikiwa imecheza michezo mitano wakiwa pointi nane nyuma ya vinara wa msimu huu na mahasimu wao Fenerbache.

Mancini iwapo atatangazwa kuchukua nafasi ya Terim atakuwa na kibarua cha kuhakikisha Galatasaray inaendeleza ubabae wake kwenye ligi ya nyumbani sanjari na mashindano ya Kombe la Ulaya kwa ngazi za Klabu.