SOKA-UEFA-ARSENAL-NAPOLI

Wenger atoa onyo kali kwa Wachezaji wake kuelekea Mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Napoli

Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger akizungumza na wanahabari na kutoa onyo kwa wachezaji wake kabla ya mchezo dhidi ya Napoli
Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger akizungumza na wanahabari na kutoa onyo kwa wachezaji wake kabla ya mchezo dhidi ya Napoli

Kocha Mkuu wa Vinara wa Ligi Kuu nchini Uingereza Arsenal, Arsene Wenger ametoa onyo kwa wachezaji wake kuwa makini kwenye mchezo wao wa siku ya jumanne wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya watakapovaana na Napoli kutoka nchini Italia. Wenger amewataka wachezaji wake kuwa na tahadhari kwa ajili ya mchezo huo kutokana na kiwango cha Napoli kuwa kizuri na iwapo hawatakuwa makini basi huenda wakapoteza mchezo huo utakaopigwa nyumbani kwao huko kwenye Dimba la Emirates.

Matangazo ya kibiashara

Onyo la Wenger linakuja baada ya Arsenal kuendelea kujichimbia kileleni mwa Ligi Kuu nchini Uingereza kufuatia kupata ushindi wake wa magoli 2-1 mbele ya Swansea kwenye mchezo uliopigwa siku ya jumamosi.

Wenger wamewataka wachezaji wake kuhakikisha hawabweteki kwa mafanikio ambayo wameyapata katika msimu huu kutokana na kufanya vizuri kwenye michezo yao na hivyo wanapaswa kuendelea kuwa makini kwenye mchezo huo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Napoli inayonolewa na Kocha wa zamani wa Liverpool, Inter Milan na Chelsea Rafael Benitez imeendelea kuwa kikosi mahiri kwenye Ligi Kuu nchini Italia maarufu kama Serie A kitu ambacho kinazidi kumuogopesha Wenger.

Benitez na Mshambuliaji wa Kimataifa wa Argentina Gonzalo Higuain aliyeshindwa kusajiliwa na Arsenal watakwenda Emirates huku wakiwa na nia ya kudhihirisha ubora walionao ni kitu ambacho kimethibitishwa na Wenger.

Wenger amekiri Benitez ni Kocha bora kabisa na ndiyo maana aliweza kuisaidia Chelsea kushinda Kombe la Europe licha ya kwamba aliichukua Timu hiyo kwa mkataba wa muda mfupi aliweza kufanya kazi yake ipasavyo.

Kocha huyo wa Arsenal amesisitiza kuwa mchezo huo wa jumanne utakuwa mgumu lakini amesema itakuwa muhimu sana iwapo kikosi chake kitashinda na kujikusanyia pointi sita kwenye michezo yake miwili.

Arsenal na Napoli wote walishinda kwenye michezo yao ya kwanza la Ligi ya Mabingwa ambapo walizifunga Marseille na Borusia Dortmund na kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua ya mtoano.