SOKA-REAL MADRID- FC COPENHAGEN-UEFA

Real Madrid kukosa huduma ya Mshambuliaji wake Gareth Bale kwenye mchezo dhidi ya FC Copenhagen kutokana na majeraha

Timu ya Madaktari wa Real Madrid wakitoa huduma ya matibabu kwa Mshambuliaji Gareth Bale
Timu ya Madaktari wa Real Madrid wakitoa huduma ya matibabu kwa Mshambuliaji Gareth Bale

Kikosi cha Real Madrid kinatarajiwa kukosa kwa mara nyingine huduma na Mshambuliaji wake ghali zaidi duniani Gareth Bale anayekabiliwa na majeraha ya nyamaza za paja na hivyo hatakuwepo kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya FC Copenhagen.

Matangazo ya kibiashara

Bale aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania maarufu kama La Liga kwenye mchezo ambao Real Madrid iliambulia kichapo cha goli 1-0 mbele ya Atletico Madrid siku ya jumamosi.

Mshambuliaji huyo mwenye thamani ya pauni milioni 85 ameendelea kuandamwa na majeraha tangu amejiunga na Real Madrid akitokea Tottenham kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili.

Bale tangu amejiunga na Real Madrid hajawahi kucheza kwa dakika zote tisini za mchezo na kwa mara ya kwanza aliondolewa katika kikosi cha kwanza baada ya kuumia wakati wa kupasha moto viungo kabla ya kucheza na Getafe.

Kocha Mkuu wa Real Madrid atalazimika kumtumia Isco kuziba pengo la Bale katika kuendelea na mkakati wake wa kusaka pointi ili kutinga hatua ya mtoano wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Bale alifanyiwa tathmini ya kubaini maumivu aliyokumbana nayo ili kujua atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani kitu ambacho kitaendelea kuigharimu timu hiyo baada ya kutumia fedha nyingi kunasa saini yake.

Real Madrid itashuka dimbani hii leo kucheza mchezo wake wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya FC Copenhagen ikiwa na kumbukumbu za kupata ushindi mnono kwenye mchezo dhidi ya Galatasaray.

Katika hatua nyingine Nahodha wa Timu ya Taifa ya Hispania na Real Madrid Mlinda mlango Iker Casillas anatarajiwa kurejea langoni kuchukua nafasi ya Diego Lopez anayekabiliwa na majeraha.

Casillas amepoteza nafasi ya kwanza kwenye kikosi cha Real Madrid kwa kile kinacholezwa kiwango chake kushuka katika siku za hivi karibuni na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Lopez.