SOKA-UINGEREZA

Chelsea yaifunga Arsenal mabao 2 kwa 0 na kufuzu robo fainali ya michuano ya Capital One

Klabu ya soka ya Chelsea imefuzu katika hatua ya robo fainali ya michuano ya kuwania taji la Capital One nchini Uingereza baada ya kuifunga Arsenal mabao 2 kwa 0 Jumanne usiku.

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo ulichezwa katika uwanja wa nyumbani wa Arsenal wa Emirates, huku Juan Mata akiifungia Chelsea bao lake la kwanza msimu huu katika kipindi cha pili cha mchuano na kuihakikishia timu yake ushindi baada ya bao la kwanza kutiwa kimyani na Cesar Azpilicueta katika kipindi cha kwanza.

Wachambuzi wa soka wanasema juhudi za wachezaji wa kiungo cha Kati wa Chelsea Michael Essien na John Obi Mikel kumiliki mpira katika eneo hilo lilisadia sana vijana wa Kocha Jose Mourinho kupata ushindi huo wa kuridhisha.

Mchuano huo wa Jumanne usiku ni wa pili kwa Arsenal kufungwa nyumbani baada ya kushindwa kutamba katika uwanja wao mwezi Februari mwaka huu, na kushindwa kwao kumetamatisha ndoto yao ya kunyakua taji hilo la Capital One ambalo wamekuwa wakilisaka kwa miaka minane sasa.

Huu ulikuwa mchuano wa kwanza wa kwa kocha Mourinho kucheza dhidi ya mwenzake Arsene Wenger tangu mwaka 2007.

Mabadiliko ya wachezaji nane yaliyofanywa na Wenger katika mchuano huo yanaelezwa na wachambuzi wa soka kuwa chanzo cha vijana wake kufungwa.

Mbali na mchuano huo, Birmingahm City walitoka sare ya kufungana mabao 4 kwa 4 na Stoke City, na baadaye Stoke City ikafanikiwa kufuzu kwa kushinda Birmingahm City kwa mikwaju ya penalti 4 kwa 2.

West Ham ilifuzu baada ya kuifunga Burnley mabao 2 kwa 0, Leicester City ikaishinda Fulhma mabao 4 kwa 3.

Manchester United nayo iliigaragaza Norwich City mabao 4 kwa 0.

Siku ya Jumatano Newcastle itamenyana na Manchester City, Tottenham Hotspurs nayo ichuane na Hull City.