SOKA

Al Ahly yataja kikosi kitakachowakabili Orlando Pirates ya Afrika kusini mwishoni mwa juma hili mjini Cairo

Kocha Mkuu wa klabu ya soka ya Al Ahly ya nchini Misri, Mohamed Yousef ametaja kikosi chake kitakachojiandaa kwa maandalizi ya kushuka dimbani kukabiliana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Al Ahly watakuwa wenyeji wa fainali za michuano ya kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika CAF itakayofanyika jijini Cairo jumapili ya mwishoni mwa juma hili.

Matangazo ya kibiashara

Wachezaji walioitwa wengi wao ni wale waliokuwa Afrika Kusini katika mchuano wa mzunguko wa kwanza kuwania taji hilo iliyopigwa Novemba 2 katika uwanja wa Orlando jijini Johannesburg.

Mtanage huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, matokeo ambayo hayakupokelewa vyema na wenyeji wa Afrika Kusini.

Amr Gamal and Ahmed Nabil Manga wametupwa nje ya kikosi hicho, wakati Ahmed Fathy na Mahmoud Abu El Saoud waliokuwa majeruhi tayari wameishapona na wamejumuishwa katika kikosi hicho.

Mshindi wa mchuano huo ataliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya dunia ya klabu bingwa, itakayofanyika kati ya tarehe 11 hadi 21 mwezi ujao nchini Morroco.