SOKA-ULAYA

Kocha wa Barcelona akiri kwamba timu yake ilijiamini sana na kupuuzia mchezo wake dhidi ya Ajax

Kocha wa Barcelona Gerardo Martino
Kocha wa Barcelona Gerardo Martino mirror.co.uk

Kocha wa Barcelona Gerardo 'Tata' Martino amekiri kwamba timu yake ililegeza kamba katika mchezo kati yake na Ajax kwa kuamini kwamba tayari imefuzu katika hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa ambapo kwa mara ya kwanza wamepoteza mchezo mmoja msimu huu baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-1 kutoka kwa timu ya Ajax jana Jumanne. 

Matangazo ya kibiashara

Barcelona ilichakazwa na wenyeji wa mchezo huo Ajax katika nusu ya kwanza ya mchezo wakati magoli kutoka kwa Thulani Serero na Danny Hoessen kuifanya timu yao kuongoza kwa magoli 2-0.

Katika kipindi cha pili Barcelona ilipata nafasi ya kuweza kufufuka na kusawazisha magoli hayo katika dakika za mwanzoni za kipindi hicho wakati Joel Veltman alipotolewa nje kwa kumchezea vibaya Neymar ndani ya eneo la hatari na Xavi kupunguza nusu ya magoli kwa kufanikiwa kutikisa nyavu za Ajax na kuiandikia timu yake goli moja.

Hata hivyo pamoja na Ajax kuwa na wachezaji 10 pekee, Barcelona ilishindwa kupata sare na hivyo kujikuta wameangukia pua kwa mara ya kwanza katika michezo 21 waliyoicheza tangu Martino alipoanza kukionoa kikosi hicho.

Bamoja na matokeo hayo Barcelona bado inaendelea kuongoza katika kundi H na inahitaji alama moja dhidi ya Celtic,katika mchezo wa fainali huko Camp Nou ili kuhakikisha kwamba inamaliza ya kwanza katika kundi hilo.