Msumbiji yaaga michuano ya CHAN baada ya kufungwa na Nigeria mabao 4-2

Timu ya taifa ya soka ya Nigeria ilipata ushindi wake wa kwanza katika michuano inayoendelea ya CHAN nchini Afrika Kusini kwa kuifunga Msumbiji mabao 4 kwa 2, lakini huu ulikuwa mchuano wa pili wa super Eagles baada ya kupoteza mchuano wa kwanza dhidi ya Mali walikofungwa mabao 2 kwa 1 Jumamosi iliyopita.

RFI
Matangazo ya kibiashara

Katika mchuano wa jana, Msumbiji ndio walikuwa wa kwanza kufua safu ya mabao kupitia mkwaju wa adhabu uliotiwa kimyani na Dario Khan katiaka dakika ya 10 ya mchuano huo.

Dakika moja baada ya bao hilo la Msumbiji, Ifeanyi Ede aliisawazishia Nigeria baada ya kupiga shuti la chini na kumpita Kipa wa Msumbiji.

Mabao mengine ya Nigeria yalitiwa kimyani na Rabiu Ali alifunga mabao mawili, huku Barnabas Omenger akiwapa vijana wa Kocha Stephen Keshi bao la nne.

Bao la pili la Msumbiji lilitiwa kimyani na Antonio Alberto Diogo.

Katika mchuano mwingine uliochezwa jana wenyeji Afrika Kusini walitoka sare ya bao 1 kwa moja na Mali.

Hii inaama kuwa kundi la A linaongozwa na Afrika Kusini kwa alama 4, ikifuatwa na Mali pia kwa alama 4, Nigeria ni ya tatu kwa alama 3 na Msumbiji ambayo ni ya mwisho bila ya alama tayari wamondolewa katika michuano hiyo na wanasubiri mchuano wa mwisho dhidi ya Mali kabla ya kupanda ndege na kurudi jijini Maputo.

Leo, kutakuwa na mechi za kundi B ,Zimbabwe watachuana na Uganda katika uwanja wa Athlone kuanzia saa kumi na moja kamili saa za Afrika ya kati na baadae Burkinafaso watamenyana na Morroco kuanzia sa mbili usiku saa za huko Afrika ya Kati.

Morroco, Zimbabwe na Burkinafaso wanatahili kushinda mechi za leo ili kujipa matumaini ya kusonga mbele.

Kesho, Ghana watachuana na Libya na Ethiopia wamalize kazi na Congo Brazaville.