AFRIKA KUSINI-CHAN

Afrika Kusini : Mechi za nusu fainali katika michuano ya CHAN zarindima

Moja ya viwanja ambako zitachezwa mechi za fainali, mjini Blomfoiten nchini Afrika Kusin
Moja ya viwanja ambako zitachezwa mechi za fainali, mjini Blomfoiten nchini Afrika Kusin RFI

Michuano ya nusu fainali ya kuwania taji la soka barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka katika ligi za nyumbani zinachezwa leo katika uwanja wa Free State mjini Blomfoiten nchini Afrika Kusini. Zimbabwe na Libya ndio watakaokuwa wa kwanza kushuka dimbani kumenyana katika mchuano wa kwanza wa nusu fainali kuanzia saa kumi na moja kamili saa za Afrika ya Kati.

Matangazo ya kibiashara

Zimbabwe ilifuzu katika hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2 kwa 1 dhidi ya Mali katika mchuano wa robo fainali uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika mchuano huo, Zimbabwe waliutawala mchezo huo na kupata mabao yao katika dakika za kwanza ya mchuano huo katika vipindi vyote viwili.

Libya nao waliwafunga Gabon mabao 4 kwa 2 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa 1 katika muda wa kawaida na wa ziada na kuzilazimu timu hizo mbili kupiga penalti.

Mchuano mwingine unaosubiriwa leo ni kati ya Nigeria wanaoshiriki kwa mara ya kwanza katika kipute hiki watashuka dimbani kumenyana na Ghana.

Ghana ilifuzu baada ya kuifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa bao 1 kwa 0, huku Nigeria ikiifunga Morroco mabao 4 kwa 3.

Kocha wa Nigeria Stephen Keshi atakuwa anawaongoza vijana wake katika mchuano huu akiwa na matumaini ya kufanya vizuri kutokana na Super Eagles kuwa na historia nzuri nchini Afrika Kusini na itakumbukwa mwaka uliopita aliiisaidia Nigeria kunyakua taji la timu barani Afrika katika michuano ya AFCON.

Washindi wa nusu fainali ya leo watamenyana katika mchuano wa fainali siku ya Jumamosi katika uwanja wa Capetown.