SOKA-MICHUANO YA KLABU BINGWA UEFA

Paris Saint-Germain yatamba uwanjani

Ezequiel Lavezzi, mchezaji wa klabu ya PSG akifurahia ushindi wa klabu yake.
Ezequiel Lavezzi, mchezaji wa klabu ya PSG akifurahia ushindi wa klabu yake. REUTERS/Gonzalo Fuentes

Vlabu vya soka vya Paris Saint Germain ya Ufaransa na Real Madrid ya Uhispania vimepata ushindi mkubwa katika michuano ya kwanza ya robo fainali ya kuwania taji la klabu bingwa barani Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Paris Saint Germain wakiwa nyumbani katika uwanja wao wa Parc des Princes walipata ushindi mkubwa wa mabao 3 kwa 1 dhidi ya Chelsea ya Uingereza.

Bao la kwanza la Paris Saint Germain limetiwa kimyani na Ezequiel Lavezzi katika dakika ya 3 ya mchuano huo, na bao la pili likatiwa kimyani baada ya David Luiz Moreira Marihno kujifunga.

Javier Pastore aliiipa klabu hio ya Ufaransa bao la tatu na la ushindi katika dakika 93 ya mchuano huo huku bao pekee la kufuta machozi la Chelsea likitiwa kimyani na Eden Hazard kupitia mkwajuu wa Penalti katika dakika ya 27.

Kocha wa Chelsea Jose Mourihno amesema mabeki walisababisha timu yake kufungwa katika mchuano huo wa kwanza ugenini, na sasa wanahitaji kupata angalau mabao 2 kwa bila ili kufuzu katika mchuano wa nusu fainali.

Aidha, Mourihno ameshtumu bao la tatu walilofungwa kwa kile anachokisema kuwa bao hilo lilikuwa la mzaha.

Mreno huyo alimchezesha mshambuliaji Andre Schurrle na kumuacha Fernando Torres huku Samwel Eto akikosa mchuano huo kwa sababu ya kuwa na jeraha la mkono.